• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
Mpango wa Tottenham kumwajiri kocha Antonio Conte watibuka

Mpango wa Tottenham kumwajiri kocha Antonio Conte watibuka

Na MASHIRIKA

TOTTENHAM Hotspur wamesitisha mipango ya kumteua Antonio Conte, 51, kuwa kocha wao mpya.

Mkufunzi huyo wa zamani wa Chelsea alitarajiwa kuwa kizibo cha Jose Mourinho baada ya matumaini ya Spurs kumwajiri upya Mauricio Pochettino aliyeyoyomea Ufaransa kudhibiti mikoba ya Paris Saint-Germain (PSG) kutibuka.

Hata hivyo, majadiliano kati ya Conte na vinara wa Spurs yametamatika ghafla huku ripoti zikiarifu kwamba hakuna uwezekano wowote wa mazungumzo hayo kurejelewa.

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Italia, Conte alikuwa na shaka kuhusu kiwango cha bajeti ambayo Spurs wangempa kwa ajili ya kusajili wanasoka wapya katika soko la uhamisho.

Huku Conte akifahamika pakubwa kwa mazoea ya kujinyakulia wanasoka wazoefu sokoni, Spurs chini ya mwenyekiti Daniel Levy, wamekuwa wakiongozwa na falsafa ya kuwakuza wachezaji chipukizi na kuwatumia kukisuka kikosi. Hilo ni jambo ambalo Pochettino alifaulu pakubwa kulifanya kambini mwa kikosi hicho.

Kutibuka kwa mpango wa Spurs kumwajiri Conte kunasaza kikosi hicho katika kibarua cha kuendelea kusaka kocha mpya, wiki saba tangu Mourinho atimuliwe mnamo Aprili 19, 2021. Mikoba ya sasa ya Spurs inashikiliwa na aliyekuwa mchezaji wa wa Spurs, Ryan Mason.

Julian Nagelsmann wa Bayern Munich na Brendan Rodgers wa Leicester City walikuwa miongoni mwa wakufunzi wengine wa haiba kubwa waliokuwa wakihusishwa na mikoba ya Spurs.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Wanavyuo kupokea ufadhili wa wa Sh4.5 milioni kutoka kwa...

Simba SC yatangaza rasmi kutalikiana na Kahata, kiungo huyo...