• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Wanawake 300 wanaokabiliwa na makali ya njaa wapata afueni

Wanawake 300 wanaokabiliwa na makali ya njaa wapata afueni

Na TITUS OMINDE

ZAIDI ya wanawake na wasichana 300 ambao wako katika hatari kubwa ya njaa kutoka North Rift wamepata afueni baada ya Jumuiya Women Fund kuwasajili kwa mpango wa kupokea fedha za kununua chakula kwa muda wa miezi sita ijayo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa hazina hiyo mjini Eldoret Winy Jeptoo, Mwenyekiti wa Bodi ya hazina hiyo alisema mpango huo unalenga kusaidia wanawake na wasichana ambao wako hatarini zaidi kushughulikia ukosefu wa usawa wa kijinsia kwa kuwawezesha kupata chakula ili kuafikia usalama wa chakula.

Bi Jeptoo alisema hazina hiyo imeweka mikakati ya muda mrefu ili kuwawezesha wanawake na wasichana waliolengwa kuwa na kumakinika kijamii na kiuchumi.

“Kupitia mradi huu tunanuia kukuza uwezeshaji wa wanawake na wasichana kwa kukabiliana na hali za dharura zinazoathiri wanawake, wasichana na watoto,” alisema Bi Jeptoo.

Jeptoo alisema mradi huo wa majaribio wa wanawake na wasichana 300 umenufaisha kaunti sita eneo la North Rift.

Hazina inatoa kwa mwezi Sh6, 000 kwa kila mwanamke anayelengwa kupitia vikundi 14 vya wanawake.

“Tunafadhili vikundi 14 vya kujisaidia vinavyoongozwa na wanawake na mashirika ya kijamii, yanashughulikia mada mbalimbali – kutoka usawa wa kijinsia hadi afya ya uzazi, haki za kiuchumi na uwezeshaji miongoni mwa nyingine,” alisema Bi Jeptoo.

Kulingana na afisa huyo, wingi wa familia zilizo hatarini zimekuwa zikikabiliwa na njaa kwa miaka miwili iliyopita kutokana na mavuno duni baada ya kipindi kirefu cha kiangazi na ukame.

Walengwa walichaguliwa kwa uangalifu baada ya kupokea hamasisho kuhusu matumizi ya fedha hizo kwa muda wa miezi sita ijayo.

Vile vile, walifundishwa mbinu za kilimo kinachozingatia hali ya hewa ili kujizalishia chakula zaidi.

Mary Losiritei mwenye umri wa miaka 64 kutoka kitongoji duni cha Turkana Boma, Kaunti ya Uasin Gishu ni miongoni mwa walionufaika.

Bi Losiritei alipongeza Jumuiya Fund kwa msaada huo akisema kwamba kabla ya usaidizi huo alikuwa akikabiliwa na umaskini wa kupindukia.

“Msaada huu ulitumwa na Mungu. Sasa nina matumaini ya kupata chakula kesho na baadaye nikijua kwamba nina chakula cha kunidumisha mimi na familia yangu,” akasema.

Msaada huo kwa wanawake walio katika mazingira magumu umefanikiwa kupitia wadau mbalimbali.

Hazina ya Usawa kutoka nchini Canada, Safaricom ni miongoni mwa washikadau wengine ambao wamefanikisha mradi huo.

Kaunti sita ambazo zinanufaika na mradi huo wa pesa ni Uasin Gishu, Nandi, Elgeyo Marakwet, Kericho, Baringo na West pokot.

 

  • Tags

You can share this post!

Jubilee Party: Mrengo wa Kanini Kega wamng’oa Uhuru

Uhuru Kenyatta atemwa na Jubilee

T L