• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Uhuru Kenyatta atemwa na Jubilee

Uhuru Kenyatta atemwa na Jubilee

Na WANGU KANURI

ALIYEKUWA Mwakilishi wa Kike katika Kaunti ya Murang’a, Bi Sabina Chege ameteuliwa kama kiongozi wa chama cha Jubilee.

Bi Sabina aliteuliwa baada ya aliyekuwa kiongozi, rais mstaafu, Uhuru Kenyatta kusimamishwa.

Kwa mujibu wa kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho ambaye bado ni Mwakilishi wa Kenya katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) Kanini Kega, Kamati ya Kitaifa ya Nidhamu nchini (NDC) iliamua kumsimamisha Bw Kenyatta kwa sababu ya mienendo yake.

Bw Kega alisema kuwa kiongozi huyo wa chama alienda kinyume na katiba ya chama alipochapisha gazetini kuwa kutakuwepo na mkutano na maafisa waliosimamishwa kazi.

Baraza Kuu la Kitaifa la Jubilee (NEC) lilisema kuwa notisi ya tarehe 28 Aprili mwaka huu haikutangazwa na katibu mkuu wa chama kulingana na katiba.

Wiki jana, Bw Kenyatta alitembelea makao makuu ya chama cha Jubilee yaliyoko Kileleshwa muda mchache baada ya mafarakano kushuhudiwa baina ya kambi ya Katibu Mkuu Jeremiah Kioni Bw Kega.

Bw Kenyatta alimtaka kiongozi yeyote anayetaka kugura aondoke bila kusababisha mgongano chamani.

“Yeyote anayetaka kuhama chama aondoke na kujiunga na kingine kwa amani. Ninawashukuru wote kwa kulinda chama chetu. Hatuna vita na yeyote na tunachowaambia wale wasiotaka kuwa katika chama hiki wako huru kuondoka na sio kuvuruga watu wenye amani hapa,” akasema Bw Kenyatta.

Vile vile, alilaumu polisi, akiwaambia wazingatie kazi yao ya kulinda umma badala ya kutumiwa kisiasa na kuzua ghasia.

“Polisi wako na kazi nyingi na sio kuja hapa kuzua ghasia. Tunaonya wale wanaojaribu kutwaa chama kwa nguvu kwamba tutakilinda,” akaongeza.

Pia alisema kwamba, wanachama wa Jubilee wanaweza kutatua tofauti zao bila kusukumwa na polisi kuhusu wanachopaswa kufanya. “Ninaomba Wakenya waishi kwa amani. Tusikubali kuchochewa.”

 

  • Tags

You can share this post!

Wanawake 300 wanaokabiliwa na makali ya njaa wapata afueni

Alice Wangui Munyua: Mtaalamu wa afya na mwandishi hodari

T L