• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 8:50 AM
WANDERI KAMAU: Tukomeshe unyama huu kwa vijana wa Kenya

WANDERI KAMAU: Tukomeshe unyama huu kwa vijana wa Kenya

Na WANDERI KAMAU

JE, ni makosa kuwa kijana nchini? Ni makosa kujihusisha na shughuli za ujana? Ni makosa kuvaa kwa mitindo ya ujana?

Pengine hayo ndiyo maswali ambayo huenda yakaibuka kutokana na mtindo ambao umekuwa ukionekana nchini—kama ni dhambi kuwa kijana.

Kwa majuma kadhaa yaliyopita, vijana wamekumbana na kila aina ya ukatili kutoka kwa jamii kwa kusingiziwa kuwa wahalifu.

Cha kusikitisha ni kuwa, fasiri hizi zinatokana na mitindo ya kimaisha ya vijana, jinsi walivyovaa na mitindo ya lugha zao.

Tukio la kwanza linahusu ndugu wawili—Benson Njiru, 22, na Emmanuel Mutura, 19, waliouawa kikatili na polisi.Ndugu hao, wanaotoka eneo la Kianjokoma, Kaunti ya Embu, wanadaiwa kuteswa hadi kufa na polisi baada ya kupatikana wakikiuka masharti yaliyowekwa kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Wawili hao walitoweka katika hali tatanishi mnamo Agosti 1, ijapokuwa miili yao ilipatikana na mmoja wa jamaa yao siku mbili baadaye katika mochari moja eneo hilo.

Mkasa uo huo ndio unaowaandama barobaro wanne—Fred Mureithi (30), nduguye mdogo Victor Mwangi (25) na binamu wao wawili, Mike George (29) na Nicholas Musa (29). Wanne hao waliuawa kikatili na wenyeji wa eneo la Ia Isinya, Kaunti ya Kajiado, kwa tuhuma za kuwa washukiwa wa wizi wa mifugo.

Walifanyiwa ukatili huo licha ya kujitetea vikali na kuonyesha kuwa wao hawakuwa washukiwa.Mwelekeo huu ni wa kusikitisha sana, hasa wakati huu ambapo nchi inaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Karibu kila uchaguzi mkuu unapokaribia tangu 1992, vijana wamekuwa wakionekana kama wahalifu.Dhana hii hutokana na baadhi yao kukubali kutumiwa na wanasiasa kushiriki katika vitendo vya uhalifu, kama vile kuvuruga mikutano ya kisiasa ya wapinzani wao.

Ingawa si wote hukubali kuingizwa kwenye vitendo na makundi hayo, jamii hujenga dhana mbaya sana kuwahusu.

Ijapokuwa makala haya hayalengi kuwatetea au kuwatakasa vijana wanaotumika kufanya vitendo vya uhalifu, ni vizuri wanajamii kutathmini kwanza kabla ya kuchukua sheria mikononi mwao.

Ni wazi kuwa tangu mfumo wa vyama vingi kuanza nchini, mchipuko wa makundi ya uhalifu umekuwa jambo la kawaida kila baada ya miaka mitano.

Baadhi ya makundi hayo ni ‘Mungiki’ (katika eneo la Kati), ‘Sungusungu’ (Kisii), Taliban, Kamjesh, 42 Brothers (mitaa ya mabanda ya Nairobi) kati ya mengine.

Kando na kutumika na wanasiasa, makundi hayo pia yameshiriki katika vitendo vingi sana vya ukatili kama mauaji, wizi wa mabavu, utekajinyara na hata ubakaji.

Hilo ni miongoni mwa sababu kuu ambapo jamii imekuwa ikiapa kuyakabili pindi inapopata nafasi, kwani polisi wamekuwa wakilaumiwa kwa kutoyakabili ifaavyo.

Hata hivyo, wakati umefika kwa jamii kufahamu kuwa si vijana wote wanaoshabikia mitindo ya kisasa ya kimaisha ni wahalifu.Wengine wanajipatia fedha kutokana na mitindo hiyo.

Hizo ndizo ajira zao—kwa mfano kusuka nywele au kuchora miili yao. Wakati umefika kwa jamii kuwakumbatia vijana kama nguzo kuu ya mustakabali wake.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Brentford wasajili kipa Alvaro Fernandez kutoka Uhispania

KINYUA BIN KING’ORI: Uchaguzi wa Zambia uwe kielelezo...