• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Wasichana 6 watimuliwa shuleni kwa mihadarati

Wasichana 6 watimuliwa shuleni kwa mihadarati

Na FAITH NYAMAI

WASICHANA sita wamefukuzwa kutoka Shule ya Sekondari ya Karen C, Nairobi, kuhusiana na madai ya kuuza mihadarati shuleni humo, huku wazazi wao wakikanusha shutuma hizo.

Wazazi wa wasichana hao walishutumu walimu kwa kuwajeruhi na kuwadhuru watoto wao.

Wakizungumza Jumamosi, wazazi hao walisema walipokea simu kutoka shuleni humo wakiagizwa kwenda kuwachukua kwa sababu walikuwa wamefukuzwa baada ya kupatikana wakichuuza dawa za kulevya shuleni.

Hata hivyo, walipowasili shuleni jana asubuhi, walisema walizuiwa kuingia shuleni ili kuzungumza na mwalimu mkuu na kuagizwa kuwasubiri watoto wao nje ya shule.

“Nilishtuka kuona binti yangu akiwa amejeruhiwa kiasi cha kutoweza kutembea, nililazimika kumpeleka hospitalini na nimeripoti kisa hicho kwa polisi,” alisema mzazi wa mtoto mmoja.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Beatrice Otieno alithibitisha kwamba wasichana sita walifukuzwa shuleni humo baada ya kupatikana wakishiriki ulanguzi wa mihadarati shuleni.

Hata hivyo, Bi Otieno, alikanusha kwamba wasichana hao walipigwa na kujeruhiwa na walimu jinsi ilivyoripotiwa akisema wanafunzi na wazazi wanaolalamika wanataka tu kuhurunmiwa.

Kupitia barua zilizoonekana na Taifa Jumapili, kila msichana alipatiwa siku yake ya kurejea shuleni.

“Mpendwa mzazi, binti yako ametumwa nyumbani kwa kosa la kupenyeza na kuchuuza mihadarati shuleni,” ilisema barua iliyotiwa sahihi na Naibu Mwalimu Mkuu.

You can share this post!

Serikali kujengea wahasiriwa Laikipia makazi

Vyakula vinavyoimarisha afya ya macho