• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 4:40 PM
Wasiwasi wakulima wa mahindi kugeukia miwa

Wasiwasi wakulima wa mahindi kugeukia miwa

Na BARNABAS BII

HATUA ya wakazi wa maeneo ambayo hufahamika sana kwa ukuzaji wa mahindi katika kaunti za Trans-Nzoia, Uasin Gishu na Nandi kukumbatia kilimo cha miwa, kimefanya utawala wa kaunti hizo kuweka sera ya kuwazuia kushiriki kilimo cha mimea mingine.

Kaunti hizo tatu sasa zimekumbatia sera ya kuhakikisha kwamba wakulima wa mahindi na ngano hawakumbatii kilimo cha miwa. Gavana wa Trans Nzoia Dkt Patrick Khaemba alisema kuwa kilimo cha miwa kitakuwa na athari mbaya kwa uzalishaji wa mbegu nzuri za mahindi eneo hilo.

“Chanzo cha kilimo huwa ni mbegu zinatotoka mashambani. Iwapo wengi watatumia mashamba yao kwa kilimo cha miwa, sehemu kidogo ya mashamba itakayobaki haitasaidia kutoa mbegu zinazostawi vizuri,” akasema Dkt Khaemba huku akisema kuwa watahakikisha sera hizo zinatekelezwa kikamilifu.

“Wale ambao wanashawishi watu wapande miwa ni wale wanaotaka wawe maskini. Unaweza kuona vyema jinsi ambavyo umaskini umekolea katika maeneo yanayokuza miwa kwa wingi,” akaongeza Dkt Khaemba.

Waziri wa Kilimo wa Trans Nzoia Mary Nzomo alisema kuwa kilimo cha miwa kinatumia ekari 5,000 za ardhi katika eneo hilo huku ekari nyingine 2,000 pia ikitayarishwa kwa kilimo hicho, jambo ambalo limezua wasiwasi kwamba wakazi huenda wakaasi kilimo cha mahindi milele.

“Hali hii ni tishio kwa kaunti hii ambayo ni ghala la chakula na ambayo pia hutoa asilimia 90 za mbegu za mahindi zinazotumika kote nchini,” akasema Bi Nzomo.

“Tumeeleza Wizara ya Kilimo iingilie suala hili na kuwazuia wakulima kushiriki kilimo cha miwa kwa sababu iwapo kitaruhusiwa kiendelee basi nchi hii haitakuwa na usalama wowote wa chakula,” akaongeza.

Kilimo cha miwa kimeanza kushamiri sana katika maeneo ya Kwanza, Saboti na Endebes katika kaunti hiyo huku tani za miwa zilizozalishwa zikipanda kutoka 1,644,395 hadi 1,041, 780 msimu uliopita.

Ardhi ambayo imetumika kwa kilimo cha miwa pia imeongezeka kutoka ekari 56.8 hadi 64.2 huku kila ekari ikitoa tani 2,198.

Ujenzi wa kiwanda cha sukari cha Butali pamoja na kukarabatiwa kwa kile cha Muhoroni na Chemelil umewashaajisha wakulima katika kaunti za Kericho, Nandi, Uasin Gishu na Trans Nzoia wakumbatie kilimo cha miwa.

“Kuna ufanisi mkubwa wa kilimo cha miwa katika maeneo hayo hasa Nandi Kusini, Tinderet na Belgut kutokana na rotuba inayopatikana,” ikasema ripoti ya kilimo iliyotolewa mnamo Mei.

Wakulima kutoka Nandi Kusini wamekuwa wakiwasilisha miwa yao kwa kiwanda cha Butalii huku wale kutoka Kericho, Kepkelion, Belgut, Tindiret na Trans-mara wakiwasilisha miwa yao kwa viwanda vya Sony, Muhoroni na Chemelil.

Viwanda hivyo, hulipa Sh4,200 kwa kila tani ya miwa, suala ambalo limechangia wakulima wengi waasi kilimo cha mahindi.

kwa kuwa fedha hizo ni za juu na pia kilimo cha mahindi kinakumbwa na matatizo ya malipo kucheleweshwa na bei duni.

You can share this post!

Posta Rangers yaipiga Gor Mahia

TAHARIRI: Kafyu: Mwelekeo wahitaji busara