• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:10 PM
Wataka fidia iwepo viumbebahari wakiwajeruhi

Wataka fidia iwepo viumbebahari wakiwajeruhi

Na KALUME KAZUNGU

WATU waliojeruhiwa na wanyama hatari wa baharini katika Kaunti ya Lamu, wamelalama kutelekezwa na serikali hasa kwa masuala ya fidia.

Waathiriwa hao ambao wengi ni wavuvi, wamesema kuwa licha ya kuvamiwa na wanyama kama vile papa, yeda na nyoka wa baharini, ambapo baadhi yao wamefariki wengine wakipoteza viungo vya mwili na kuachwa na makovu ya milele, Shirika la Huduma za Wanyama Pori (KWS), eneo hilo, halijawasaidia.

Wavuvi hao badala yake wamekashifu KWS kwa kuangazia sana migogoro ya binadamu na wanyama pori pekee.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Usimamizi wa Wavuvi (BMU), Kaunti ya Lamu, Bw Mohamed Somo, alisema kuwa familia za wanachama wake walioangamizwa na viumbe wa baharini , zinaishi kifukara kwa kukosa fidia.

“Kuna kamati ya Kaunti ambayo hushughulikia masuala ya fidia. Tunashangaa kwamba kamati hiyo inaangazia tu masuala ya fidia kwa wanaoumizwa na wanyama pori ilhali sisi tunaong’atwa na viumbe hatari baharini tumetelekezwa,” akasema Bw Somo.

Bw Shee Kombo, 50, ambaye ni mkazi wa kisiwa cha Kiwayu, Lamu Mashariki ni mmoja wa wavuvi ambaye kwa sasa amesalia nyumbani akiuguza jeraha la mguu baada ya kuumwa na yeda.

Bw Kombo anasema si mara ya kwanza kwake kuumwa na mnyama huyo hatari wa baharini lakini hakuna hatua yoyote imechukuliwa na KWS kumfidia au kumsaidia kwa matibabu hospitalini.

Alisema amewahi kupiga ripoti mara kadhaa kwa KWS kuhusiana na kesi yake lakini hadi sasa amepuuzwa.

“Juni 17, mwaka jana, niliumwa na yeda wakati nikivua samaki baharini eneo hilo la Kiwayu. Nilikaa nyumbani miezi sita nikiuguza jeraha. Mwaka huu Juni 4 nikaumwa tena na yeda na hadi sasa nimekaa nyumbani nikifuatilia matibabu hospitalini. Mguu wangu umelemaa na licha ya kupiga ripoti kwa KWS, sijapata usaidizi wowote,” akasema Bw Kombo.

Bw Mohamed Bakari, ambaye pia ni mwathiriwa, anaeleza kuwa hajapokea usaidizi wowote tangu alipong’atwa na mkunga akivua samaki baharini.

Mwenyekiti wa kundi la wavuvi (BMU) eneo la Kiwayu, Bw Adam Lali alisema miaka mingi pia imepita tangu baadhi ya wanachama wake walipoumwa na mkunga, yeda na papa na hadi sasa kesi zao hazijashughulikiwa.

Hata hivyo, mwenyekiti wa kamati ya fidia kwa waathiriwa wa wanyama pori na viumbe wa baharini, Kaunti ya Lamu, Bw Ali Shebwana, alipuuzilia mbali madai kwamba wanaoumizwa na wanyama wa baharini eneo hilo, wamekuwa wakitelekezwa.

Bw Shebwana alisema mwezi Juni mwaka huu, serikali ilitoa takriban Sh8 milioni ili kuwafidia waathiriwa wa wanyama pori, ambapo visa vitatu kati yake vilikuwa vya wale walioumizwa na wanyama wa baharini.

Naye afisa wa KWS, Kaunti ya Lamu, Bw Mathias Mwavita, aliwahimiza waathiriwa kupiga ripoti kwa ofisi yake haraka punde wanapojeruhiwa au kuuawa na wanyama hao ili makadirio yafanywe na wapate kufidiwa.

You can share this post!

MARY WANGARI: Kenya yahitaji mbinu za kisasa kuboresha...

Kagwe atishia kuadhibu walipishao chanjo