• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 12:18 PM
Watano washtakiwa kwa ulaghai wa simu

Watano washtakiwa kwa ulaghai wa simu

Na RICHARD MUNGUTI

MFANYAKAZI wa kampuni ya Safaricom ni miongoni mwa watu watano walioshtakiwa kwa ulaghai wa kadi ya simu Safaricom uliopelekea kampuni moja kupoteza Sh3 milioni.

Sabastiam Ogutu Owino, Albert Agala Oyondi, Joran Kyalo Wambua, Alex Kipkoech Kigen na Kevin Maina walishtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi Robinson Ondiek kwa ulaghai wa mtandao wa kadi za simu.

Wote wanakabiliwa na shtaka la kuibia kampuni ya Millan Access Capital Company Limited Sh3milioni kati  ya Januari 24-26, 2023.

Kyalo na Maina wanakabiliwa na mashtaka ya kupatikana na Sh317, 250 wakijua zimepatikana kwa njia ya ukora.

Kyalo alidaiwa alikutwa na polisi akiwa na Sh265, 000 na Maina akiwa na Sh52, 250 wakijua zimepatikana kwa njia isiyo halali.

Washtakiwa hao waliachiliwa kwa dhamana ya Sh100, 000 pesa tasilimu kila mmoja.

Mawakili Shadrack Wamboi na Danstan Omari waliwakilisha washtakiwa hao ambao kiongozi wa mashtaka hakupinga ombi lao kuachiliwa kwa dhamana.

Awali Omari alikuwa amepinga hatua ya polisi kuwatumia washtakiwa ujumbe mfupi wakiwataka wafike kortini kujibu shtaka.

“Ujumbe mfupi wa simu almaarufu SMS sio mojawapo ya njia zinazotambuliwa kisheria kuwatumia washtakiwa kufika kortini kujibu mashtaka,” alisema Bw Omari.

Hakimu alikubaliana na Omari kwamba SMS sio utaratibu unaotambuliwa kisheria kuwataka washukiwa kufika kortini.

Kesi itatajwa Mei 2, 2023 kutengewa siku ya kusikizwa.

  • Tags

You can share this post!

Serikali yatangaza Ijumaa, Aprili 21, 2023 kuwa siku ya...

Mmiliki wa Chelsea atishiwa maisha baada ya Real Madrid...

T L