• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Wawili wanaswa kufuatia mkasa wa kufa maji kwa watahiniwa Uasin Gishu

Wawili wanaswa kufuatia mkasa wa kufa maji kwa watahiniwa Uasin Gishu

NA TITUS OMINDE

Maafisa wa upelelezi katika Kaunti ya Uasin Gishu wamewakamata washukiwa wawili kuhusiana na mkasa wa maafa ya watahiniwa watano wa mtihani wa mwaka huu wa Darasa la Nane, KCPE.

Watahiniwa hao walifariki baada ya kuzama kwenye bwawa la maji.

Washukiwa wakuu ni wamiliki wa eneo hilo la burudani.

Kamanda wa polisi Kaunti ya Uasin Gishu Benjamin Mwanthi alithibitisha kukamatwa kwa washukiwa hao ambao ni wakurugenzi wa The Amazement Park ambao ni pamoja na Nixon Koimur na mkewe Gladys Chepchirchir.

Watahiniwa hao walifariki siku moja kabla ya kufanya mtihani wao ambao ulianza leo, Oktoba 30, 2023.

“Tumewakamata wakurugenzi wawili wa The Amazement Park kuhusiana na kisa cha watahiniwa watano wa KCPE walizama kwenye bwawa katika burudani yao,” alisema Bw Mwanthi.

Wakurugenzi hao walikamatwa muda mfupi baada ya kuhojiwa katika kituo cha Polisi cha Burnt Forest.

Kukamatwa kwao kuliwadia baada ya Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki na mwenzake wa Elimu Ezekiel Machogu kuagiza kukamatwa mara moja kwa wale wanaohusishwa na tukio hilo.

Bw Machogu mnamo Jumapili Oktoba 29 alisema idara yake inashirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani kuhakikisha uchunguzi wa kina kuhusu kisa hicho cha kusikitisha unafanywa.

“Hatua zinazofaa zitachukuliwa dhidi ya washukiwa baada ya uchunguzi. Walimu, wazazi na walezi wanashauriwa kuepuka kuweka wanafunzi hasa mazingira hatari,” akaonya Bw Machogu.

Watahiniwa watano kati ya 185 wa Shule ya Msingi ya Arap Moi ambao walikuwa wafanye mitihani ya kitaifa ya Darasa la Nane na Darasa la Sita walifariki baada ya kuzama kwenye bwawa lililotengenezwa na binadamu walipokuwa safarini katika bustani ya burudani, kilomita sita kutoka taasisi hiyo.

Kilichoanza kama kujitenga na shughuli za kawaida za kujitayarisha kwa mtihani huo kiligeuka kuwa mkasa baada ya wavulana saba wa darasa la nane kujitenga na timu nyingine bila taarifa ya walimu wao na kuamua kupanda boti.

Lakini katika muda usiozidi dakika 10 watano kati yao walikuwa wamelala kwenye ufuo wa bwawa wakiwa wamekufa huku mwingine akiwa amepoteza fahamu baada ya kuzama.

Wazazi na maafisa wa Wizara ya Elimu waliotembelea shule hiyo Jumapili walinyimwa kuingia shuleni kutokana na kile maafisa wa usalama walichokitaja kuwa ulinzi wa watahiniwa kwa mateso zaidi ya kiakili.

Ndugu wa watoto waliofariki waliendelea kusimulia nyakati zao za mwisho na walioathirika kabla ya msiba huo.

“Nilikuwa na mazungumzo marefu ya kutia moyo na kaka yangu siku ya Jumatano na kuahidi kupata zaidi ya alama 370 kwa nia ya kujiunga na Starehe Boys na kuwa daktari siku zijazo lakini hilo halitatimia sasa. Ndoto hizo zimekatizwa na kisa cha kuzama majini,” akakumbuka Naomi Chepchumba.

  • Tags

You can share this post!

Boresha afya: Haya ni baadhi ya matumizi mengi ya ndizi

Wapalestina waliouawa Gaza sasa wafikia 8,000

T L