• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Wapalestina waliouawa Gaza sasa wafikia 8,000

Wapalestina waliouawa Gaza sasa wafikia 8,000

DEIR AL-BALAH, GAZA

NA MASHIRIKA

MAMIA ya malori Jumapili yaliingia katika ukanda wa Gaza, yakiwa yamebeba misaada kusaidia maelfu ya Wapalestina walioathiriwa na mashambulio yanayoendelea kutekelezwa na ndege za kivita za Israeli.

Hata hivyo, wafanyakazi wa mashirika ya kimisaada walisema kwamba misaada hiyo haitoshi, ikilinganishwa na idadi kubwa ya watu wanaohitaji misaada ya bidhaa za matumizi ya kimsingi.

Maelfu ya watu waliripotiwa kuvamia maghala ya kuweka misaada na kupora unga na bidhaa nyingine za matumizi ya msingi.

Hayo yalijiri huku Wizara ya Afya eneo la Gaza ikisema kuwa zaidi ya Wapalestina 8,000 wameuawa tangu vikosi vya Israeli kuanza kutekeleza mashambulio ya angani dhidi ya maeneo yanayoaminika kuwa ngome za wanamgambo wa Hamas.

Wizara hiyo ilisema kuwa wengi kati ya wale waliofariki ni watoto na wanawake.

Kufikia sasa, Israeli imewapoteza watu 1,400 kwenye mashambulio hayo, maafa mengi yakitokana na shambulio lililotekelezwa na Hamas dhidi ya raia wake Oktoba 7.

Mnamo Jumapili, vikosi vya Israeli vilianza mashambulio makali ya ardhini dhidi ya kundi la Hamas katika ukanda wa Gaza, katika kile Waziri Mkuu wa taifa hilo, Benjamin Netanyahu, alitaja kuwa “mwanzo mpya wa mashambulio” dhidi ya kundi hilo.

Netanyahu alisema kuwa taifa hilo litafanya kila liwezalo kulisambaratisha kabisa kundi la Hamas. Kwa karibu wiki tatu, wakazi katika ukanda huo wamekuwa wakiishi gizani, bila umeme, baada ya Israeli kukata mitambo ya kusambaza umeme.

Israeli pia ilikata huduma za mawasiliano na mtandao wa intaneti, hali iliyofanya mawasiliano katika ukanda huo kuwa magumu.

Kukatwa kwa huduma za mawasiliano kuliathiri sana shughuli za uokoaji, kwani ilikuwa vigumu kwa waokoaji kuwafikia watu walioathiriwa na mashambulio ya angani ambayo yamekuwa yakitekelezwa kwa ndege za kivita za Israeli.

Hata hivyo, hapo jana, mashirika kadhaa ya habari katika ukanda huo yaliropoti kuwa huduma za mawasiliano ya simu na mtandao wa intaneti zimerejea kama ilivyokuwa hapo awali.

Netanyahu aliwaonya raia wa Israeli kutarajia “operesheni kali na ndefu ya kijeshi” dhidi ya ukanda huo. Hata hivyo, baadhi ya washirika wameishauri Israeli kusitisha kwa muda operesheni hiyo ya mashambulio ya ardhini.

Ijapokuwa jeshi lilionekana kuanza operesheni hiyo pole pole, kinyume na ilivyokuwa imetangazwa hapo awali, Netanyahu aliapa kufanya kila awezalo kuwaokoa zaidi ya Waisraeli 200 wanaoendelea kushikiliwa na kundi la Hamas kama mateka.

Mateka hao pia wanajumuisha raia kadhaa wa kigeni.“Hii ndiyo awamu yetu ya pili ya vita vyetu, ambavyo lengo lake kuu li wazi: kulivuruga kabisa kundi la Hamas na kuwarejesha nyumbani mateka linaowashikilia,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Wawili wanaswa kufuatia mkasa wa kufa maji kwa watahiniwa...

Ten Hag aning’inia pembamba Man United wakiyumba...

T L