• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:35 AM
Waziri wa Maji Alice Wahome aapa kushuka na wanaomchimba kisiasa

Waziri wa Maji Alice Wahome aapa kushuka na wanaomchimba kisiasa

NA MWANGI MUIRURI

WAZIRI wa Maji, Bi Alice Wahome ameapa kuwa atafanya juu chini ikiwemo kupiga siasa ili elinde wadhifa wake.

Bi Wahome alisema kuwa wanaompiga vita ni watu wabinafsi katika Kaunti ya Murang’a ambao wanataka kutawala sekta ya maji ili kujinufaisha.

“Baadhi yao wanafikiria kuwa watapata mamilioni kutoka kwa ujenzi wa mabwawa yaliyopendekezwa kwa kunipiga vita. Wanasahau kuwa Rais William Ruto anapigana na ufisadi,” akasema Bi Wahome.

Kadhalika, waziri huyo alisema amechoka kuamka kila siku kukutana kukabiliana na masuala ambayo yanaweza kushughulikiwa katika vikao vya mashauriano na mazungumzo.

“Inafikia wakati lazima tuheshimiane na kusonga mbele kama jamii. Mimi ni mwanasiasa mzoefu na sina upungufu wa ujanja wa hapa na pale. Hii ndio maana nataka tuzungumze na tuwatumikie watu wetu…lakini ikiwa kuna wale wanaoleta masuala ya kisiasa, basi hata mimi bado nina umaarufu kisiasa,” akaongeza Bi Wahome.

Katika muda wa wiki mbili zilizopita, Mbunge wa Maragua Mary wa Maua na mbunge mwakilishi wa wanawake Betty Maina wamemshtumu waziri huyo kwa kuvuruga ajenda ya utoaji wa maji katika kaunti hiyo.

Bi Wa Maua alipanga maandamano dhidi ya waziri huyo ambapo wito wa kufutwa kazi ulitolewa.

Vita hivyo vilienea hadi kwenye mitandao ya kijamii ambapo Bi Maina alitangaza kuwa “kuna mtu ambaye ofisi yake itafungwa na rais hivi karibuni”.

“Msifikirie kuwa sina umaarufu kisiasa kwa sababu mimi ni waziri. Mimi ndiye waziri ambaye aligombea kiti cha ubunge cha Kandara na kushinda mihula mitatu,” alisema.

Akizungumza katika ukumbi wa Kenol Town’s Christian Foundation Fellowship church, Bi Wahome alisema, “kuna wale wanaoshinikiza nifutwe kwa matumaini kwamba watateuliwa kuchukua nafasi yangu. Ninatafuta kuwashauri wanasiasa hao kuchunga maneno yao na pia kutambua kwamba tabia hiyo ya makabiliano haitawapeleka popote katika ngazi ya uongozi wa kaunti”.

Alisema wanachama wengine wanaolenga kuleta maendeleo ni Naibu Rais Rigathi Gachagua, Waziri wa Biashara Moses Kuria, Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wa, Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro na Mbunge wa Naivasha Jane Kihara.

“Nilijitolea na kustahimili mashambulio makali ya Rais Uhuru Kenyatta, tulishinda na kuunda serikali na tunapostahili kutulia kufanya kazi kwa ajili ya wananchi, hapa Murang’a vita vidogo vinazuka.”

Bi Wahome alisema, “vita vinafanya iwe vigumu kwangu hata kuzuru baadhi ya maeneo kutokana na mtazamo hasi wa wabunge wa eneo hilo kunihusu na kuchapisha matamshi ambayo yanalenga kunidhalilisha”.

Seneta wa Murang’a Joe Nyutu ambaye aliandamana na Waziri huyo alisema kuwa Rais Ruto ana wasiwasi kuwa waziri wake anapigwa vita nyumbani.

  • Tags

You can share this post!

Muumini wa Kanisa la Kiadventista aponyoka na Sh11 milioni...

Usiku wa UEFA ambao Man Utd na Arsenal waliona giza

T L