• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Usiku wa UEFA ambao Man Utd na Arsenal waliona giza

Usiku wa UEFA ambao Man Utd na Arsenal waliona giza

PARIS, Ufaransa

Mashabiki walishuhudia matokeo ya kushangaza Jumanne usiku timu maarufu za Manchester United na Arsenal ziliposhindwa kuwika mbele ya limbukeni katika mechi za makundi za kuwania ubingwa Klabu Bingwa barani Ulaya (UEFA).

Matokeo ya kushangaza zaidi yalishuhudiwa ugani Old Trafford, wenyeji Manchester United walichapwa 3-2 na Galatasaray kutokana na mabao ya Wilfried Zaha, Mohammed Kerem Akturkoglu na Mauro Icardi, wakati Rasmus Hojlund akifungia wenyeji mabao yote.

Kufuatia matokeo hayo, timu hiyo ya kocha Erik ten Hag lazima ifanye kazi ya ziada na kushinda mechi zilizobakia ili kufutua ndoto yao ya kusonga mbele katika mashindano hayo ya UEFA.

Manchester wako mkiani mwa Kundi A baada ya kushindwa 4-3 na vinara Bayern Munich katika mechi ya utangulizi.

Itabidi wapate ushindi katika mechi ijayo ili wafufue matumaini ya kutinga raundi ya 16 Bora.

Kitumbua chao kiliingia mchanga zaidi, baada ya kiungo wao Carlos Casemiro kuonyeshwa kadi nyekundi dakika ya 77 baada ya kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.

Manchester watakutana na FC Copenhagen katika mechi ijayo mnamo Novemba 29, siku ambayo Galatsaray itaalika Bayern Munich jijini Istanbul nchini Uturuki.

United hawakuwa na ubavu wa kukabiliana na Galatasaray hasa katika kipindi cha pili baada ya Casemiro kutolewa, lakini kocha ten Hag ana matumaini kwamba timu yake itafanya vyema katika mechi ya marudiano.

Kwingineko, licha ya kutangulia kuona lango kupitia kwa bao la Gabriel Jesus, kocha Mikel Arteta alishuhudia vijana wake wakichapwa 2-1 ugenini na Lens ya Ufaransa.

Jesus alifunga bao lake mapema dakika ya 14, lakini matumaini yake yakazimwa na mabao ya Adrien Thomasson na Elye Wahi waliofunga dakika za 25 na 69 mtawaliwa.

Licha ya kichapo hicho, kocha Arteta aliipongeza Lens kwa ushindi wao huku akikisifu kikosi hicho cha kocha Franck Haise kutokana na soka safi kilichoonyesha.

Kiungo mshambuliaji, Bukayo Saka aliumia na kuondolewa uwanjani katika mechi hiyo iliyochezewa ugani Bollaert-Delelis. Huenda nyota huyo akakosa mechi ya EPL dhidi ya Manchester City.

Lakini kiungo Declan Rice alisema matokeo hayo yamemponza kwa vile yameifanya timu hiyo kuteremka hadi nafasi ya pili nyuma ya Lens, huku akiongeza kipigo hicho kimetia azma timu yake kuongoza kundi la B.

Bayern wanaongoza Kundi A kwa pointi sita, wakifuatiwa na Galatasaray. Lens walio na pointi nne ndio vinara wa Kundi B mbele ya Arsenal kwa tofauti ya pointi moja.

Kundi C linamilikiwa na Real Madrid wanaojivunia pointi sita, mbele ya Napoli walio na tatu, sawa na Braga. Real Sociedad na Inter Milan zinashikilia nafasi mbili za kwanza katika Kundi B, kila moja ikiwa na pointi nne.

Matokeo ya mechi zilizochezwa Jumanne yalikuwa: Lens 2 Arsenal 1, Napoli 2 Real Madrid 3, Manchester United 2 Galatasaray 3, Copenhagen 1 Bayern Munich 2, PSV Sevilla 2, Inter Milan 1 Benfica 0, Union Berlin 2 Braga 3, RB Slazburg 0 Real Sociedad 2.

  • Tags

You can share this post!

Waziri wa Maji Alice Wahome aapa kushuka na wanaomchimba...

Mudavadi apokonya Mutua wizara ya Mashauri ya Kigeni kwenye...

T L