• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Wito watafiti washirikiane na idara za afya kuongoza uundaji wa sera bora

Wito watafiti washirikiane na idara za afya kuongoza uundaji wa sera bora

MKAMBURI MWAWASI Na JURGEN NAMBEKA

WASHIKADAU wa sekta ya afya Pwani wamewataka watafiti wa sekta mbalimbali kushirikisha idara za afya za kaunti kufanya utafiti, ili kuhakikisha kuwa matokeo ya utafiti yanachangia kwa kutengenezwa kwa sera zenye ufaafu.

Akizungumza katika hafla ya kupokea vifaa vya thamani ya Sh 600,000 vya kusaidia katika utafiti wa athari za Covid-19 kwa wafanyakazi wa afya wa kike, Waziri wa afya kaunti ya Mombasa Bi Swabah Ahmed alitaka watafiti washirikiane na kaunti kwa kuwa tayari idara hizo zina data.

“Kutoka kwa utafiti huu tunaoanza kushiriki leo na Chuo Kikuu cha Aga Khan na shirika la utafiti la IDRC, kaunti yetu itaweza kupata matokeo itakayotuwezesha sisi kujiandaa kwa majanga mengine endapo yatatokea. Kushirikishwa kunahakikisha kuwa kama kaunti tutakuwa na uwezo wa kutumia matokeo ya utafiti kuunda sera zitakazotumika,” akasema Bi Ahmed.

Bi Pauline Oginga anayefanya kazi katika wizara ya afya kaunti ya Mombasa, alieleza kuwa kaunti ilikuwa na data ya kutosha ambayo ingewezesha watafiti kufanya utafiti wenye ufaafu.

Kulingana na kiongozi wa utafiti huo Prof Marleen Temmerman kutoka Chuo Kikuu cha Aga Khan, utafiti huo unalenga kubaini iwapo kulikuwepo na tofauti katika athari za Covid-19 baina ya wanaume na wanawake wanaofanya kazi katika sekta ya afya.

“Tungependa kufanya utafiti huu baina ya wafanyikazi wa afya wa kike na wa kiume ili tuweze kubaini ni tofauti gani za athari za janga la Covid-19 na kujipanga iwapo kutatokea janga lingine nyakati zijazo,” alisema.

Bi Marleen pia aliongeza kwamba shughuli hiyo iliyoanza na kaunti za Mombasa na Kilifi, inanuiwa kufanyika katika kaunti nyingine za Pwani zikiwemo Kwale, Lamu, Tana River na Taita Taveta.

Aliongeza kwamba ni  vyema kwa wizara ya afya katika serikali ya kaunti na ya kitaifa kuzingatia afya ya kiakili ya wafanyakazi wa huduma za afya.

“Ni vyema wafanyakazi wa afya kuangaliwa maslahi yao kwa kuzingatia kwamba wao ndio huwa nyanjani na wangonjwa. Kwa kushughulikia afya yao ya kiakili itasaidia kunawirisha sekta ya afya nchini,” alisema.

  • Tags

You can share this post!

Okutoyi kuongoza Team Kenya kwenye mashindano ya tenisi ya...

Mfanyabiashara ashtakiwa kwa wizi wa mbolea ya Sh6 milioni

T L