• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 1:14 PM
Yesu wa Tongaren mafichoni akidaiwa kukataa ‘kufia dhambi za Wakenya’

Yesu wa Tongaren mafichoni akidaiwa kukataa ‘kufia dhambi za Wakenya’

NA SAMMY WAWERU

MHUBIRI anayejitambua kama Yesu Wa Tongaren, kutoka Kaunti ya Bungoma Ijumaa amedaiwa kuenda mafichoni kufuatia tishio la wakazi ‘kumsulubisha’. 

Huku jamii ya Wakristu kote ulimwenguni ikianza kuadhimisha Sikukuu ya Pasaka, wenyeji wa Tongaren wamesema wanataka kubainisha endapo mtumishi huyo wa Mungu ni Yesu wa ukweli au bandia.

Wakiongozwa na wahudumu wa bodaboda, wameapa kumsulubisha sawa na alivyosulubishwa Yesu Kristu.

Sikukuu ya Pasaka huadhimishwa kila mwaka duniani na Wakristu, kama ukumbusho wa kusulubishwa kwa Yesu Kristu mwana wa Mungu.

Yesu alisulubishwa pamoja na wezi watatu, na siku ya tatu akafufuka.

“Leo tumeamua tutamsulubisha Yesu wa Tongaren. Ikiwa si Yesu wa ukweli, tutamtwanga viboko,” akasema mmoja wa wakazi hao.

Ni kufuatia tishio hilo mhubiri huyo ambaye majina yake halisi ni Eliud Simiyu, aliamua Ijumaa kuchana mbuga na kuenda mafichoni kuokoa maisha yake.

Kilichoanza kama mzaha miezi, majuma na siku kadha zilizopita wakazi kutishia kumsulubisha kinaashiria kuwa kutaka kutimia.

Mapema mwaka huu, Taifa Leo iliangazia mhubiri huyo mwanachama na kiongozi wa Kundi la New Jerusalem, katika kijiji cha Lukhokwe, ambapo alidai kwamba ni jumla ya watu 168, 000 kote duniani wataenda mbinguni.

Kilichozua ucheshi zaidi, Nairobi kulingana na Bw Simiyu ni watu wawili pekee watakaouona Ufalme wa Mungu na isitoshe hawajazaliwa.

Baadaye, Yesu wa Tongaren alidai hutazama mbingu kati ya saa mbili asubuhi hadi saa sita mchana na kuzungumza na malaika.

Sawa na alivyokuwa Yesu Kristu, mchungaji huyo ana mitume, kila mmoja akiwa na majina ya kipekee.

Kwa mujibu wa Biblia, Yesu Kristu hakuoa, ila Yesu wa Tongaren ameoa na ana watoto wanane.

Mhubiri huyo anadai Yesu Kristu aliyetabiriwa na Isaiah, anapaswa kuoa na kupata familia.

Hadi kufikia wakati wa kuchapisha taarifa hii, haikuwa imebainika alikojificha huku duru zikiarifu ameyoyomea Uganda.

Aidha, awali alikuwa ameibua taharuki kuhusiana na tishio la wanakijiji kumsulubisha.

  • Tags

You can share this post!

Alikatwa mguu mmoja, awachenga wasio na ulemavu

Gavana alia wizi wa maji 001

T L