• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Alikatwa mguu mmoja, awachenga wasio na ulemavu

Alikatwa mguu mmoja, awachenga wasio na ulemavu

NA KALUME KAZUNGU

MSEMO wa ulemavu si kutoweza unadhihirishwa kikamilifu na mwanasoka maarufu wa Lamu, Lucky Hinzano Mzee,31.

Bw Hinzano alizaliwa kijiji cha Boko, tarafa ya Witu, kaunti ya Lamu mnamo 1992.

Yeye ni mzawa wa pili katika familia ya watoto watatu, wakiwemo wavulana wawili na msichana mmoja.

Bw Hinzano na wenzake waliachwa mayatima wakiwa na umri mdogo baada ya wazazi wao kufariki.

Kulingana na Bw Hinzano, mapenzi yake kwa mchezo wa kandanda yalianza akiwa tumboni.

Anasema alianza kucheza mpira punde tu alipoanza kusimama dede kijijini kwao, akipiga mateke kila kitu kilichokuwa mbele yake, iwe ni kikombe, sahani, nakadhalika.

Tabia yake iliwasukuma wazazi kumuundia tufe na kumpa kuanza kucheza akiwa na furaha za mpwitopwito.

Hali hiyo ilimfanya kutambua na kukienzi mapema kipaji chake cha kandanda.

Alipofika umri wa miaka tisa mnamo 2002, Bw Hinzano aliugua maradhi ya maradhi ya baridi yabisi almaarufu arthritis, hali iliyopelekea yeye kufanyiwa operesheni na kukatwa mguu wake wa kushoto.

Hapo ndipo alipong’amua kuwa safari yake ya kutaka kuwa mwanasoka tajika nchini na ulimwenguni ilikuwa imeingia doa jeusi na karibu izame kabisa katika kaburi la sahau.

Baada ya upasuaji na mguu kukatwa, Bw Hinzano alipewa mikongojo ya kumsaidia kutembea.

Alikaa nyumbani kwa muda wa miaka miwili, akijifunza kutembea kwa mikongojo na pia kujihoji ni vipi kipaji chake atakiendeleza licha ya kisirani kilichotua maishani mwake.

Mwaka wa tatu, Bw Hinzano akapiga moyo konde….,liwe liwalo, akahiari kurudi uwanjani kusakata kandanda na mguu mmoja kwa usaidizi wa mikongojo.

Kwa sasa yeye amekuwa mashuhuri, akicheza pamoja na wasio walemavu kisiwani Lamu.

Kila ukimshuhudia akicheza, Bw Hinzano huwa jasiri na mwenye bidii, akielekeza fikra zake zote kwenye mpira. Ukimwona jinsi anavyowachenga na kuwapepeta wenzake uwanjani utadhani yeye hana ila yoyote ila ana miguu yote miwili.

Kitakachopelekea wewe kujua huyu si mchezaji wa kawaida ni mikongonjo ambayo huitumia kwa ustadi mkubwa kusaka mpira kwa wapinzani wake uwanjani, kuwachenga na kuingiza magoli ama kupeana pasi kwa wenzake.

Ni kutokana na umashuhuri wa mwanasoka huyu katika kusakata kandanda ambapo amejizolea sifa kochokocho, hivyo kuibuka kupendwa na wengi ndani na nje ya Lamu.

Jitihada zake zilipelekea yeye kutauliwa kuchezea klabu ya walemavu ya Mombasa Amputee Football Club International yenye makazi yake jijini Mombasa.

Ikumbukwe kuwa Klabu ya Mombasa Amputee Football International ndiyo bingwa wa vilabu vyote 10 vipatikanavyo Kenya vya soka ya walemavu.

Bw Hinzano ni miongoni mwa wachezaji 15 na maafisa wa benchi ya kiufundi ya klabu hiyo 5 ambao watakuwa safarini kuelekea jijini Dar-es-Salaam nchini Tanzania kuanzia Aprili 24 na 25 mwaka huu wanakoenda kuwakilisha Kenya kwenye mechi za  walemavu.

Mechi hizo zitafanyika uwanja wa Uhuru Stadium, Tanzania kuanzia Aprili 29 hadi Mei 3, 2023.

Klabu ya walemavu ya Sauti Parasports ndiyo bingwa wa vilabu vya walemavu vya Tanzania na itakuwa ikikabiliana na Mombasa Amputee Football Club International kwenye michezo hiyo.

 

Kutoka Kushoto: Fahad Mohamed, Bwana Tora na Yusuf Mohamed (kulia) wakipokea uelekezi kutoka kwa Bw Lucky Hinzano Mzee (katikati na mwenye mikongojo) kabla ya kuanza mazoezi yao katika uwanja wa Kashmir Sports Ground kisiwani Lamu. Bw Hinzano ni hodari wa kusakata kandanda licha ya ulemavu wa mguu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Hinzano anashukuru kwamba licha ya kuwa mlemavu, bado ametia bidii kuona kwamba kipaji chake anakipalilia na kung’ara kila kuchao.

“Ningependa kuwashauri walemavu wengine kwamba wasijifiche majumbani bali wajitokeze. Walemavu bado wamebarikiwa na vipaji mbalimbali. Serikali za kaunti, viongozi na wahisani pia wajitokeze kuanzisha ligi za michezo ya walemavu, iwe ni kandanda, voliboli, mpira wa magongo, netiboli nakadhalika. Haya yakipewa kipaumbele ninaamini walemavu wengi watajitokeza kustawisha vipaji vyao,” akasema Bw Hinzano.

Aliwashauri wazazi wenye watoto walemavu kukoma kuwaficha ndani ya majumba yao na badala yake wawaache huru ili waonekane na vipaji vyao kutambuliwa na kupaliliwa.

“Kwa mfano, wazazi wangu au mimi mwenyewe ningeamua kujifungia ndani ya nyumba eti kwa sababu ni mlemavu, singeweza kupiga zile hatua nilizozifikia sasa. Inasikitisha kuwa Lamu hakuna vilabu wala nyanja za walemavu, hivyo kutulazimu sisi wenye upungufu wa viungo kucheza na wasio na ulemavu. Ningemsihi Gavana, Issa Timamy kuwapa walemavu kipaumbele, hasa kimichezo,” akasema Bw Hinzano.

Katibu Mkuu wa Klabu ya Mombasa Amputee Football International ambayo Bw Hinzano huchezea, Bw Geoffrey Kamande Kariuki alimtaja Bw Hinzano kuwa shujaa na hodari katika kusakata kandanda ya walemavu.

Bw Kamande alisema klabu yake huzienzi sana huduma za Bw Hinzano ambaye hucheza safu ya beki nambari mbili au mara nyingine nambari saba.

Alitaja baadhi ya changamoto zinazokabili klabu hiyo, ikiwemo ukosefu wa fedha, vifaa vya kuchezea nakadhalika.

“Hawa wachezaji walemavu wanahitaji mikongojo maalum ya kuchezea soka, jezi na vinginevyo vingi ili kufaulisha vipaji vyao. Kwenda Tanzania tayari tunahitaji karibu Sh6.5 milioni na hatuna chochote. Tungewasihi wahisani, viongozi na wengineo kuingilia kati tusaidiwe tusikose michezo ya walemavu Tanzania mwezi huu,” akasema Bw Kamande.

Kufaulisha safari hiyo, klabu ya Mombasa Amputee Football International imeanza kuchangisha kupitia Mchango, Paybill 891300, akaunti namba ikiwa ni 67314.

“Wachezaji 15 na maafisa wa kiufundi 5 tutahitajika kuwa safarini kuelekea Tanzania kuanzia Aprili 24 na 25. Tukisaidiwa kuchangisha kupata fedha za usafiri na matumizi tutashukuru,” akasema Bw Kamande.

Bw Hinzano alisomea shule ya msingi ya Boko iliyoko Witu kati ya mwaka 2003 hadi 2011.

Alijiunga na Shule ya Sekondari ya Witu kati ya 2012 hadi 2015.

Baadaye alisomea Dimploma ya Uhifadhi wa Rekodi za Afya na Usimamizi wa Mawasiliano katika taasisi ya Eldoret Technical Training Institute kati ya 2017 na 2019.

Bw Hinzano ambaye ni baba wa mtoto mmoja kwa sasa anahudumu kama afisa wa Uhifadhi wa Rekodi za Afya kwenye kituo cha afya cha Ibnusina Nursing Home and Pharmacy kilichoko mjini Lamu.

  • Tags

You can share this post!

Azimio yateua wakali meza ya majadiliano

Yesu wa Tongaren mafichoni akidaiwa kukataa ‘kufia...

T L