• Nairobi
  • Last Updated May 14th, 2024 6:55 AM
Barabara ya Broadway Thika yakaribia kukamilika

Barabara ya Broadway Thika yakaribia kukamilika

Na LAWRENCE  ONGARO

WAFANYABIASHARA wengi mjini Thika wamepongeza juhudi za wao kuundiwa barabara ya by-pass kutoka Delmonte- BAT- Broadway hadi kuunganishwa na ile kuu ya Garissa.

Mbunge wa Thika Bw Patrick Wainaina,  alisema viwanda vingi vilivyo kando ya barabara ya Broadway, vitanufaika pakubwa kibiashara.

Wakulima wengi kutoka Mlima Kenya pia watanufaika pakubwa watakapopitia barabara hiyo wakisafirisha bidhaa zao hadi sokoni.

Mbunge wa Thika Bw Patrick Wainaina. Picha/ Lawrence Ongaro

Alieleza pia kuwa wenye magari kutoka Mashariki mwa nchi watapata afueni kutumia barabara hiyo.

Aliitaja halmashauri ya mamlaka ya kuunda barabara za mijini (KURA), kama iliyoleta mabadiliko kwa wakazi wa Thika kwa ujumla.

Alisema mradi huo wa barabara utagharimu takribani Sh1.7 bilioni kufikia itakapokamilika.

Alisema eneo la BAT mjini Thika limekuwa na utata kwa sababu watu wachache walinunua ardhi eneo la barabara huku wakipinga kujengwa kwa barabara hiyo.

“Tungeiomba mahakama kufanya juhudi kuona ya kwamba kesi zilizo huko zinatolewa ili barabara ipitie hapo,” alisema mbunge huyo.

Alisema kwa muda wa miaka minane iliyopita serikali ya Jubilee imeweza kukarabati kilomita 50 za barabara eneo la Thika mjini na vitongoji vyake.

Barabara hiyo pia itasaidia malori makubwa kupitia hapo bila kukwama kama hapo awali.

“Hapo awali kulikuwa na mashimo mengi katika barabara hiyo na mvua iliponyesha kulikuwa na shida ya matope kutapakaa kote,” alifafanua mbunge huyo.

Meneja wa kampuni ya Tosha Holding Construction Ltd, Issa Ali Barre, alisema kampuni hiyo imeunda barabara ya kisasa inayoweza kuhimili malori mazito ya kubeba mizigo.

“Wamiliki wa  magari watapata nafuu wakipitia kwenye barabara hii kutokana na ubora wake. Kampuni imeunda barabara ya kiwango cha juu,” alisema meneja huyo.

Bw Douglas Chege ambaye ni mhudumu wa bodaboda alisema wameshukuru kwa kukarabatiwa kwa barabara hiyo kwa sababu watapata faida kubwa kama wanabodaboda.

” Hapo awali tulikwama kupitia kwa matope, lakini sasa tutaendelea kubeba wateja wetu mara nyingi,” alifafanua mhudumu huyo.

Alisema hata wafanyabiashara wengi watanufaika pakubwa kwa kusafirisha bidhaa zao kwa urahisi.

You can share this post!

Afueni kwa wamiliki wa baa na hoteli

Wakulima wa kahawa kusubiri zaidi viwanda vikarabatiwe

T L