• Nairobi
  • Last Updated December 2nd, 2023 1:45 PM
Afueni kwa wamiliki wa baa na hoteli

Afueni kwa wamiliki wa baa na hoteli

Na WANGU KANURI

WAZIRI wa Afya Mutahi Kagwe ametangaza kuwa baa na hoteli zitafungwa kuanzia saa tano usiku.

Bw Kagwe alitoa tangazo hilo ili kuondoa tashwishi iliyokuwa miongoni mwa Wakenya.

Hii ni baada ya Tume ya Huduma za Polisi (NPSC) kutangaza kwamba hoteli na baa zitafungwa saa moja usiku licha ya kafyu kuondolewa hapo jana Jumatano.

Vile vile Bw Kagwe alieleza kuwa itifaki zote za kunawa mikono, kutumia sanitaiza na kuweka umbali wa mita moja na nusu baina ya watu bado zitafuatwa kikamilifu.

Hali kadhalika, wamiliki wa hoteli na baa watapaswa kuhakikisha kuwa kuna vituo vya watu kunawia mikono na kuzingatia idadi ya watu.

“Leo jioni tutapokea dozi 500,000 za chanjo aina ya Johnson & Johnson na baada ya wiki mbili tutakuwa tumepokea na kusambaza chanjo zinazohitajika ili tufikie lengo letu la kuwapa chanjo watu milioni 10 ifikapo Desemba,” waziri Kagwe akaeleza.

“Lengo letu ni kuhakikisha kuwa chanjo hizo zimewafikia watu wengi kwa muda mfupi uwezekanavyo. Ninawarai Wakenya wasisite kwendea chanjo na wahakikishe kuwa wazazi wao pia wamepewa chanjo hizo,” akaongeza.

Hata hivyo, waziri huyo aliwaomba wahamasishaji katika jamii kushirikiana na wanaopatiana chanjo hizo ili kupunguza hasara.

Hii ni kwa sababu, chanjo za Pfizer na Moderna zinapaswa kutumika kabla ya siku 30 kuisha baada ya kutolewa kwenye jokofu.

You can share this post!

Kipchoge kuwania tuzo ya mwanariadha bora duniani dhidi ya...

Barabara ya Broadway Thika yakaribia kukamilika

T L