• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
El Nino: Wakazi wa South B wazibua mitaro ya majitaka

El Nino: Wakazi wa South B wazibua mitaro ya majitaka

NA SAMMY KIMATU

MAKUNDI ya Jamii yako mstari wa mbele kuhamasisha wakazi kuhusu tahadhari za mapema kukabiliana na Mvua ya El Nino katika mitaa ya mabanda ya Mukuru ilioko South B, kaunti ndogo ya Starehe, kaunti ya Nairobi.

Wiki hii, wanachama wa kikundi cha Haki Community Conservation Initiative wakiongozwa na mwenyekiti wao, Bi Dorothy Wanja walikuwa katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Sokoni kufanya usafi mtaani humo.

Wakishirikiana na makundi mengine-Concern Worldwide. Child Fund, Hand in Hand East Africa na wanafunzi wa Shule ya Kenya Kids Learning Centre walifagia, wakakusanya taka na kuzibua mitaro ya kupitisha maji taka katika mtaa wa Mukuru-Sokoni.

Akiongea na Taifa Leo katika hafla hiyo, katibu mkuu wa Haki Community, Bi Imelda Bosire alisema nia ya shughuli hiyo ilikuwa kuhamasisha wakazi mitaani umuhimu wa kudumisha usafi serikali inapojiandaa kukabiliana na athari za Mvua ya El Nino.

“Tunaonyesha wakazi kuwajibika kukoma kutupa taka ovyo tukiwasomesha kwamba taka ina mapato bali na kuwafunza kutupa taka ovyo huziba mitaro na kisha huchangia pakubwa mafuriko hasa wakati huu serikali inaonya wakenya kujiandaa mapema kuhusu mvua ya El Nino,“ Bi Bosire akasema.

Isitoshe, kabla ya zoezi la kufanya usafi mtaani, watoto wa Kenya Kids Learning Centre, waliimba nyimbo, wakatumbuiza kwa mashairi yaliyokuwa na mada kuhusu umuhimu wa kuyatunza mazingira.

Katika shughuli hiyo ya siku nzima, washiriki zaidi ya 100 walishirikiana kufanya usafi kuanzia makao makuu ya Msaidizi wa kaunti na pia katika ofisi ya chifu Hazina, eneo la Poa Poa, South B Pefa Church, Mandazi Road, River Bank na maeneo mengine mkabala wa barabara ya Aoko.

Vilevile, Bi Wanja alisema baada ya kufanya usafi, wakazi mitaani watasambaziwa mifuko ya kuweka taka ambazo zitakusanywa na kubebwa na malori kutoka serikali ya kaunti ya Nairobi kupelekwa Dandora.

  • Tags

You can share this post!

AMINI USIAMINI: Thorny devil ni mjusi ambaye hunywa maji...

Wakulima wa miwa walia njaa viwanda vikisalia vimepigwa...

T L