• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Gavana Arati ashangaza kudai baadhi ya MCA Kisii wanaogopa kusafiri kwa ndege   

Gavana Arati ashangaza kudai baadhi ya MCA Kisii wanaogopa kusafiri kwa ndege  

NA NYABOGA KIAGE

GAVANA wa Kisii Simba Arati manmo Jumapili, Agosti 20, 2023, alidai kuwa baadhi ya wawakilishi wadi (MCA) katika kaunti yake wanaogopa kusafiri kwa kutumia ndege.

Bw Arati alikuwa akimjibu mbunge wa Mugirango Kusini Bw Silvanus Osoro ambaye alilalamika kuwa gavana huyo anabagua madiwani katika safari zake kuenda ng’ambo.

Alihoji kuwa Arati anapendelea MCA wa Azimio, na kunyima fursa wale wa Kenya Kwanza kuandamana naye.

“Sio ukweli kuwa niliwaacha nyuma wawakilishi wadi wengine, huo sio ukweli. Nilisafiri na wawakilishi 51 na kuacha nyuma 21 kwa sababu wengine wanaogopa kusafiri kuabiri ndege na wengine hawakuwa na pasipoti,” gavana huyo alisema katika uwanja wa Nyanturago ulioko eneobunge la Nyaribari Chache, Kisii.

Hafla hiyo ilikuwa pia imehudhuriwa na Rais William Ruto pamoja na viongozi wengine kutoka eneo hilo.

Gavana Arati alisema kuwa alikuwa tayari kufanya kazi na Rais Ruto ili kuhakikisha kuwa maendeleo yanapelekwa katika Kaunti ya Kisii.

“Mimi kama Gavana wa Kisii niko tayari kufanya kazi na serikali kuu,” aliahidi gavana huyo.

Alikiri kuwa Rais Ruto alimshinda kinara wa upinzani, Bw Raila Odinga kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 2022.

Hata hivyo, aliomba Rais Ruto akutane na Bw Odinga ili wafanye mazungumzo kuzuia msururu wa maandamano ambayo yalishuhudiwa nchini miezi miwili iliyopita.

Gavana Arati ambaye anahudumu muhula wake wa kwanza, pia alisema kuwa Bw Odinga hakuwa anamezea mate serikali ya nusu mkate.

“Ni muhimu kujua kuwa siasa lazima iwe na adabu kiasi. Viongozi wote inapaswa tuwe na subira kwani hakuna malaika ambaye atashuka kutoka mbinguni, ni sisi ndio tutawasaidia watu wetu,” Gavana huyo alielezea.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Silvanus Osoro asema akistaafu siasa atakuwa Pasta

Barobaro anavyounda hela kama njugu kupitia uchakataji...

T L