• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 3:09 PM
Silvanus Osoro asema akistaafu siasa atakuwa Pasta

Silvanus Osoro asema akistaafu siasa atakuwa Pasta

NA SAMMY WAWERU

MBUNGE wa Mugirango Kusini, Silvanus Osoro amehoji kwamba akistaafu ulingo wa siasa atarejea kanisani kueneza injili.

Mwanasiasa huyo wa chama cha UDA, amesema Jumapili, Agosti 20, 2023 kujitolea kwake kuhudumia nyumba ya Mungu (kanisa) kumemshawishi kutaka kuwa pasta.

“Mimi nikimaliza kazi ya siasa (akimaanisha kustaafu), nitakuwa mhubiri,” akasema mbunge huyo, akizungumza katika ibada ya misa Uwanja wa Nyanturago, Kisii ambayo ilihudhuriwa na Rais William Ruto.

Dkt Ruto aliungana na wakazi Kaunti ya Kisii kuwashukuru kwa kumchagua Rais, Agosti 9, 2022.

Wengine walioandamana na Rais kutoka jamii ya Kisii, ni Waziri wa Elimu, Ezekiel Machogu, Gavana (Kisii), Simba Arati, miongoni mwa viongozi na wanasiasa wengine kutoka eneo hilo.

Bw Osoro alitumia jukwaa hilo kueleza wenyeji kwamba akiondokea siasa, kibarua atakachoingilia ni kuhubiri.

“Mimi nitaiga nyayo zako Mheshimiwa Rais, nitakuwa pasta kama unavyosema unalenga ukistaafu,” Kiranja huyo wa wengi Bunge la Kitaifa alisema.

Kilichozua ucheshi zaidi, ni kudai kwamba kinyume na wachungaji wengine wanaohadaa waumini na washirika wao, yeye atakuwa safi kama pamba.

Isitoshe, alisema hatakula sadaka.

“Na sitakula sadaka, nitazitumia vizuri,” Bw Osoro aliahidi, akidokeza kwamba yeye ni patroni wa kanisa.

Aidha, Osoro ni mcheza piano kanisani na katika hafla nyingi za kitaifa za maombi hutwikwa jukumu hilo.

Hali kadhalika, ni mwanakwaya wa kwaya ya bunge.

Mbunge huyo machachari anahudumu awamu ya pili bungeni, na ni mwandani wa Rais William Ruto.

  • Tags

You can share this post!

Mkenya aliyefariki katika ajali ya barabara Amerika...

Gavana Arati ashangaza kudai baadhi ya MCA Kisii wanaogopa...

T L