• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 1:22 PM
Barobaro anavyounda hela kama njugu kupitia uchakataji mbegu za mafuta 

Barobaro anavyounda hela kama njugu kupitia uchakataji mbegu za mafuta 

NA SAMMY WAWERU

SIRI katika kilimo ni uongezaji thamani, kuchakata mazao ya shamba.

Ikiwa safari yake katika kilimo cha mbegu za mafuta inaweza kubadilishwa na kuulizwa achague kati ya njia ya kuuza mazao au kuongeza thamani, Joshua Gitonga, mkulima kutoka Kaunti ya Meru, anasisitiza kwamba bado angechagua kuchakata (processing).

Anakuza alizeti, kanola, na soya kwenye shamba lenye ukubwa wa ekari 50 hadi 100.

Joshua Gitonga, mkulima wa mbegu kukama mafuta ya kupikia Kaunti ya Meru. PICHA|SAMMY WAWERU

Mashamba hayo yapo katika kaunti za Meru, Tana River, na Nakuru.

“Nilianza na ekari 2 mwaka wa 2014, ambapo nilitangulia na alizeti na soya,” Gitonga anafunguka.

Kulingana na mkulima huyu kijana barobaro, soko lake kuu wakati huo lilikuwa ni watengenezaji wa chakula cha mifugo.

Joshua Gitonga, akielezea kuhusu mafuta ya kupika anayochakata katika Kaunti ya Meru. PICHA|SAMMY WAWERU

Soko hilo lilikuwa na faida ndogo, anasema Gitonga, akielezea kuwa alianza utafiti ambao ulizaa matunda yenye tija.

“Niliendeleza utafiti na kugundua ninaweza kuongeza thamani mbegu za alizeti na soya kwa kuzikama mafuta, kabla ya kuzipeleka sokoni,” anasema.

Joshua Gitonga akipanga mafuta kwenye duka lake eneo la Kaari, Meru. PICHA|SAMMY WAWERU

Alianza na mashine yenye uwezo kuzalisha tani 2 kwa siku, ambayo anafichua alinunua kwa Sh500, 000.

Fedha hizo zilitoka kwa akiba yake mwenyewe na mapato.

Baadaye, Gitonga alinunua mtambo wa kuchakata tani 8 kwa siku.

Mojawapo ya mashine ambayo Joshua Gitonga anatumia kusindika mbegu za mafuta. PICHA|SAMMY WAWERU

Gitonga anaamini ukamaji mafuta ya kupika ni biashara inayoweza kuinua uchumi wa nchi, na ulimwengu kwa jumla.

Kenya inaagiza zaidi ya asilimia 90 ya mafuta ya kupikia, na bidhaa hiyo sasa inauzwa mithili ya dhahabu.

Joshua Gitonga na mmoja wa wafanyakazi wake wakitia mbegu kwenye mashine kukama mafuta ya kupikia. PICHA|SAMMY WAWERU

Gitonga, mwenye umri wa miaka 30, anakadiria mchango wake katika mtandao wa uongezaji mbegu za mafuta thamani na kuyazalisha kama asilimia 1 pekee, akisema kuwa hawezi kukidhi mahitaji ya nchi.

Ndiyo, anakubali kuwa ni mojawapo ya sekta ya viwanda ambayo haijaangaziwa kikamilifu.

Joshua Gitonga akionyesha mafuta yanayotokana na alizeti, kanola na soya, japo hayajapitia hatua zote kuyasafisha. PICHA|SAMMY WAWERU

Katika kijiji cha Chaaria, umbali wa karibu mita 100 hivi kutoka barabara kuu ya Meru – Nairobi, ana kiwanda cha kuchakata mbegu za mafuta kinachokalia kwenye nusu ekari.

Kina mashine mbili za kuchakata mafuta, zenye uwezo kukama tani 10 kwa siku.

Pia katika kituo hicho, kuna eneo la kuhifadhi mbegu za alizeti, soya, na kanola, na nafasi ya kuunda mashine za kutoa mafuta sokoni (Automated Teller Machine – ATM).

Joshua Gitonga anakotengenezea ATM za kudondoa mafuta sokoni. PICHA|SAMMY WAWERU

Biashara ya Gitonga imestawi kiasi cha kuwa na mkataba na wakulima 62, 000, kupitia programu ya kukusanya mazao ambapo hutoa huduma za mafunzo kuhusu kilimo bora na faafu.

Hata hivyo, kati ya idadi hiyo, wakulima 25, 000 ndio wanamsambazia mbegu kwa sasa.

Kila mkulima, kulingana na mwasisi huyu wa Rafikipay Ltd, kampuni aliyoanzisha mwaka wa 2018 baada ya kugura kazi katika Tume ya Huduma za Bunge (PSC) ili kuvalia njuga kikamilifu kilimo cha mbegu za mafuta, lazima awe na kipande cha shamba angalau robo ekari na ahudhurie mafunzo.

Mafuta ya alizeti, kanola na soya tayari kuingia sokoni. PICHA|SAMMY WAWERU

Aidha, mwanachama lazima atie saini mkataba wa kufuata kanuni na sheria zinazotolewa, hasa kuendeleza kilimo bora na kwa kitaalamu.

“Wakulima wananufaika moja kwa moja kupitia mpango wa kunisambazia mazao. Kama si Rafikipay, sijui wangekuwa wakipeleka mavuno yao wapi,” alisema alipohojiwa Akilimali Dijitali, wakati wa ziara katika kituo chake cha kuchakata.

Pauline Mwari, mkulima wa alizeti katika Kaunti ya Meru, ni mmoja wa wanaonufaika kupitia Rafikipay Ltd.

Joshua Gitonga na Pauline Mwari, mmoja wa wakulima wanaonufaika kupitia Rafikipay Meru. PICHA|SAMMY WAWERU

Akiwa aliingilia kilimo cha mbegu za mafuta miaka ya sabini (70), Pauline anakiri kuwepo kwa kituo hicho kunampa malipo bora ikilinganishwa na miaka iliyopita.

“Awali kabla ya kiwanda hiki kufunguliwa, kilo moja ya mazao ya alizeti ilikuwa ikinunuliwa kati ya Sh2.50 na Sh5, lakini sasa tunauza kwa zaidi ya Sh50,” anasema.

Soko lake kuu lilikuwa madalali wa alizeti.

Kupitia mpango wa mafunzo ya kilimo bora kitaalamu, Gitonga husambaza mbegu zilizoidhinishwa.

Mafuta ya alizeti, soya na kanola ambayo hayajachujwa. PICHA|SAMMY WAWERU

Aidha, mjasirimali huyu ana apu ya kidijitali ndiyo Rafiki Farmers Management, anayoitumia kutoa huduma zake.

Kwa kuwa idadi ya maafisa wa kilimo wa nyanjani wa serikali nchini inazidi kupungua, anashirikiana na wakulima 10 aliowapa mafunzo kusambaza kwa wenzao.

Mchango wake kupiga jeki wakulima wa mbegu za mafuta, mwaka wa 2022 ulimfanikisha kupata tuzo ya AYuTE Africa Challenge kutoka kwa Shirika la Heifer International.

Joshua Gitonga akionyesha tuzo ya AYuTE. PICHA|SAMMY WAWERU

Gitonga alikuwa wa pili bora katika shindano la Heifer kutambua wabunifu wanaotumia teknolojia za kisasa kuboresha kilimo, ambapo alikabidhiwa kima cha Sh500, 000.

Anafichua kwamba alitumia fedha hizo kuwekeza zaidi katika biashara yake.

“AYuTE ni mpango ambao tuliuanzisha mwaka jana, 2022, nchini Kenya, na unatambua vipaji wanaotumia bunifu za kidijitali kutatua matatizo yanayokumba wakulima katika mtandao wa uzalishaji,” anasema Esta Kamau, Mkurugenzi Mkuu Heifer Kenya.

Kutambuliwa kwangu kumenifungulia fursa nyingi, Gitonga anakiri.

Joshua Gitonga akibeba mtungi wenye mafuta anayozalisha. PICHA|SAMMY WAWERU

Kati ya wakulima 25, 000 anaoshirikiana nao kwa karibu, 21, 300 ni wanawake na vijana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 35.

Maganda ya mbegu za mafuta, huuzia viwanda vya kutengeneza chakula cha mifugo.

Lita moja ya mafuta ya alizeti huuza Sh300, kanola Sh350 na soya Sh400, bei ya jumla.

Afisa Mkuu Mtendaji huyu wa Rafikipay anasema asilimia 95 ya mafuta anayozalisha kwa kuchakata huuzia wafanyabiashara wa rejareja.

Huwapa mashine za ATM za bure.

Anasisitiza kwamba bidhaa zake ni asili, hakuna kemikali wala viungio vyovyote anavyotumia wala kuweka.

Gitonga ana wafanyakazi 12 wa kudumu, na wakati kazi inawazidi, huajiri vibarua 10, hasa wakati wa kupanda, kupalilia, kuvuna, na mafuta yanapohitajika kwa wingi.

Hata hivyo, anasema kufikia alipo haijakuwa rahisi kwani kupata mbegu bora na zilizoidhinishwa ni kibarua.

Joshua Gitonga anasema biashara ya uchakataji mafuta ya kupika ikikumbatiwa itasaidia kubuni nafasi za ajira hasa kwa vijana. PICHA|SAMMY WAWERU

Anategemea mbegu zinazonunuliwa kutoka Tanzania, Malaysia, na Ukraine kupitia wafanyabiashara wenye leseni ambao anasema huuza bei ghali sana.

Ukosefu wa vifaa vya kisasa na fedha kupanua kituo chake cha kuchakata, ili kukidhi mahitaji ya soko pia kunazuia ukuaji wake.

Gitonga kwa sasa yuko katika hatua za mwisho kupata idhini za bidhaa zake kuthibitishwa na Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa Nchini (Kebs).

“Uongezaji thamani ndio njia ya kipekee kuboresha sekta ya viwanda ambayo itasaidia kuangazia kero ya ukosefu wa ajira hasa kwa vijana.

“Wafanyabiashara na wadauhusika wanapaswa kutathmini mbinu na mifumo kuchakata bidhaa za kilimo,” anasisitiza.

Gitonga hutegemea misimu ya mvua kuzalisha mbegu za kukama mafuta.

 

  • Tags

You can share this post!

Gavana Arati ashangaza kudai baadhi ya MCA Kisii wanaogopa...

Omanyala kutia mfukoni Sh850,000 licha ya kushika nafasi ya...

T L