• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Kang’ata atia breki utoaji wa Sh4,000 kwa kila mimba Murang’a kuzima ukora

Kang’ata atia breki utoaji wa Sh4,000 kwa kila mimba Murang’a kuzima ukora

NA MWANGI MUIRURI

SERIKALI ya Kaunti ya Murang’a imesimamisha kwa muda mpango wake wa kuwapa wanawake wajawazito kiinua mgongo cha Sh4,000 kwa sababu ambazo haikufafanua.

Katika taarifa ambayo serikali hiyo ilipachika katika kurasa zake za majukwaa maarufu ya mitandao ya kijamii mnamo Desemba 20, 2023, ilisema kwamba mpango huo kwa sasa uko chini ya uhasibu na utarejelewa tena Februari 2024.

“Tangazo hili lalenga kupiga msasa mpango huo lakini malipo na usajili utaendelea huku uhasibu ukiendelea kuhusu masuala tata, kurejelewa kwa harakati za kawaida kukiwa ni Februari mwakani,” akasema Gavana Irungu Kang’ata.

Madaktari walioongea na Taifa Leo walidokeza kwamba kumeibuka visa vya utapeli ambapo baadhi ya matabibu hushirikiana na wajawazito bandia au wa uainishaji usiofaa na kudai malipo hayo.

“Tumekuwa hata na visa vya akina mama wajawazito kutoka kaunti nyingine kuja kujisajili katika Kaunti ya Murang’a huku hata wengine wasio na mimba wakitengenezewa stakabadhi za ujauzito hivyo basi kupora ushuru wa wenyeji,” akasema daktari mmoja ambaye aliomba asitajwe jina.

Mpango huo wa fidia umesifiwa na baadhi ya wazee katika jamii kama unaosaidia jamii ya eneo la Mlima Kenya–hasa Agikuyu–kupata watoto hivyo basi kujipatia idadi tosha ya wapigakura kwa hesabu za kuwa na ushawishi. Aghalabu siasa za mataifa mengi ya Kiafrika huendeshwa kwa misingi ya kikabila.

Mpango huo hutoa Sh1,000 mimba ikitinga miezi saba, kiasi sawa katika mwezi wa nane na kisha Sh2,000 mwanamke akishajifungua katika hospitali yoyote ya umma.

Bw Kang’ata alizindua mpango huo mnamo Machi 27, 2023, katika hospitali ya Kirwara iliyoko kaunti ndogo ya Kandara.

Alisema kwamba mpango huo unalenga kuwasaidia wenyeji kukumbatia afya bora ya kujifungulia hospitalini badala ya nyumbani.

  • Tags

You can share this post!

Namna ya kuandaa nyama ya mutura kulika msimu wa Krismasi

KCPE: Shule za kibinafsi zalia kuhusu uteuzi wa sekondari

T L