• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
KCPE: Shule za kibinafsi zalia kuhusu uteuzi wa sekondari

KCPE: Shule za kibinafsi zalia kuhusu uteuzi wa sekondari

NA WINNIE ATIENO

MALALAMISHI yameibuka miongoni mwa wamiliki wa shule za kibinafsi baada ya wanafunzi wa shule za umma kusajiliwa kujiunga na shule za upili za kitaifa, wengine wao wakiwa na alama chini ya 400.

Wamiliki hao wametaja hatua ya serikali kuwa ya ubaguzi wakiitaka Wizara ya Elimu kuwatendea haki watoto ambao walifanya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE) katika shule za kibinafsi.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Memon Academy iliyoko Mombasa, Joseph Ndoro, alisema hawakuridhishwa na uteuzi wa wanafunzi kujiunga na shule za upili mwaka huu.

“Wanafunzi wangu bora ambao walipata alama 400 katika KCPE wameitwa shule za upili za hapa hapa tu karibu. Nilishangaa kuona wanafunzi wangu bora ambao walipata alama 406 na 405 wakiitwa Shule ya Upili ya Wasichana ya Mama Ngina na mwenzake akipata Kenyatta High,” alisema Bw Ndoro.

Alisema kwa mara ya kwanza wanafunzi wake wamesajiliwa katika shule za Pwani badala ya zile za kitaifa zilizo Nairobi na sehemu nyinginezo za bara kama ambavyo imekuwa kawaida.

“Sijaridhishwa na usajili na namna shughuli hiyo ilivyotekelezwa. Tulidhania wanafunzi wetu bora wangeitwa shule maarufu za kitaifa kama vile Alliance High, Pangani, ama Mang’u High lakini tulishangaa sana wameitwa Kenyatta High, Mama Ngina na Ribe Girls,” aliongeza.

Walimu wenzake wakuu katika shule za kibinafsi nao walieleza kutoridhishwa na uteuzi huo wakiwataka viongozi wa kisiasa na wale wa kidini kuingilia kati suala la elimu wakisisitiza kuna dosari.

Wamiliki wengine wa shule ya kibinafsi walitoa mfano wa shule ya umma huko Mombasa ambayo wanafunzi wake 23 walipata shule za kitaifa.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Muungano wa Kitaifa wa Wazazi, Silas Obuhatsa, na Mwenyekiti wa Kitaifa wa Muungano wa Walimu Wakuu, Johnson Nzioka, walisema hakukuwa na ubaguzi kwenye uteuzi huo.

“Tunampongeza Waziri wa Elimu, Ezekiel Machogu, kwenye uteuzi huu ambao ulikuwa na usawa. Nimeona wanafunzi wote ambao walipata alama 400 wakipewa nafasi katika shule za kitaifa. Sijaona ubaguzi wowote,” alisema Bw Obuhatsa.

Bw Nzioka alisema uteuzi huo ulifanywa kwa njia ya kielektroniki.

“Tuwache kuweka dosari kwa kila jambo. Kwa mfano kama mwanafunzi alichagua Shule ya Upili ya Nyeri High ama Alliance High, halafu Alliance isajili wanafunzi kulingana na idadi yake ilhali wengi zaidi walitaka kujiunga na shule hiyo, tutalalamikia nini?” aliuliza Bw Nzioka.

Alitoa mfano wa Shule ya Upili ya Kitaifa ya Wasichana ya Pangani jijini Nairobi ambayo wanafunzi 144,542 walikuwa wanataka kujiunga nayo licha ya kuwa na nafasi ya wanafunzi 384 pekee wa Kidato cha Kwanza.

“Je tutaweza kusajili watoto wote 144,542 hapo Pangani Girls High?” aliuliza.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Muungano wa Wamiliki wa Shule za Kibinafsi, Charles Ochome, alisema bado wanaendelea kuchambua uteuzi huo.

“Ni mapema sana kutoa kauli yangu kuhusu uteuzi huu sababu bado tunaendelea kuchambua utaratibu uliotumika katika uteuzi huo. Tukimaliza tutazungumza,” alisema Bw Ochome.

Hata hivyo, waziri Machogu, alieleza kuwa baadhi ya wanafunzi wapatao 28,052 ambao walipita mtihani huo wa kitaifa hawakupokea mialiko ya kujiunga na shule zozote za kitaifa kwa sababu hawakuzichagua.

  • Tags

You can share this post!

Kang’ata atia breki utoaji wa Sh4,000 kwa kila mimba...

Mombasa yameremeta Krismasi ikibisha hodi

T L