• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 12:11 PM
Kuandaa kahawa ya kupendwa na wateja si ‘kalongolongo’

Kuandaa kahawa ya kupendwa na wateja si ‘kalongolongo’

NA KALUME KAZUNGU

KUTANA na Mzee Farid Mohamed Silaha almaarufu ‘Farid Kahawa’.

Kwa takriban miaka 25 sasa, Bw Farid amekuwa akivuma na kutamba ndani ya kisiwa cha Lamu kutokana na weledi wake wa kutengeneza na kuuza kahawa chungu.

Ikumbukwe kuwa kahawa chungu ni kinywaji kinachoenziwa si haba katika maeneo ya mwambao wa Pwani.

Katika Ukanda wa Pwani, hasa miji ya Lamu, Mombasa, Kilifi, Malindi, Mambrui na mingineyo, si ajabu kuwapata waja, hasa wazee, mara nyingi nyakati za jioni, wakiwa wamekaa mabarazani na mikekani, wakipiga gumzo huku wakibugia kahawa chungu taratibu. Utawaona wameshika majikombe ya kahawa.

Kahawa ni tunda au mbegu ya mbuni. Wakati unga wa mbegu za buni zilizokaangwa unapokorogwa kwa wingi kutumia maji hutengeneza kahawa chungu ambayo huwa rangi nyeusi tititi.

Ladha ya kinywaji hicho ni ya uchungu, hatua iliyochangia kubandikwa jina hilo la ‘Kahawa Chungu.’

Kwa mzee Farid, ambaye ana miaka 62, aidha, siri na upekee aliong’amua katika kuiandaa kahawa chungu imemfanya kudumu katika miashara hiyo miaka nenda miaka rudi.

Kila jioni inapowadia utampata Bw Farid akiwa ameweka buli au chupa zake kadhaa za kahawa chungu juu ya meza kwenye baraste ya mbele ya mji wa kale wa Lamu huku akitandaza vitafunia mbalimbali, tayari kutegea wanunuzi.

Bw Farid Silaha akihudumia wateja wake eneo la baraste ya mbele ya mji wa kale wa Lamu. Amedumu kwenye biashara ya kuuza kahawa chungu kwa zaidi ya miaka 25 sasa. PICHA | KALUME KAZUNGU

Wateja wake hujumuisha wenyeji, wageni na watalii wa ndani kwa ndani na wale wa ng’ambo.

Umaarufu alionao kama muuzaji wa hahawa chungu kisiwani Lamu umemfanya Bw Farid kubandikwa jina la msimbo ‘Farid Kahawa.’

Mara nyingi utampata Bw Farid akiwa amezingirwa na halaiki ya wateja waliokaa kwa utulivu kwenye viti katika eneo lake la kibiashara wakati akiwahudumia kwa kuwachotea kutoka kwa buli au chupa na kuwakabidhi kahawa chungu.

“Nilianza kazi hii miaka ya 1990s. Nimedumu biasharani kwa zaidi ya miaka 25 sasa na bado ninavutia wateja kila kukicha. Kuna baadhi ya marafiki tulioanzisha biashara sawa lakini wakasambaratika. Kuna wale waliojaribu kuniiga nao pia walifunga biashara zao kitambo kwa kukosa wateja. Upande wangu kila kukicha biashara inanawiri, hivyo kunilazimu kuongeza kiwango cha kahawa chungu ili kitosheleze idadi kubwa ya wateja,” akasema Bw Farid.

Je, ni nini hasa siri inayomfanya Bw Farid kudumu katika biashara ya kahawa chungu ikilinganishwa na wafanyabiashara wengine kisiwani?

Anaeleza kuwa ladha ya kahawa hulingana na jinsi mpishi anavyoshughulikia kinywaji hicho.

Aghalabu anasema kila mtu ana uwezo wa kuandaa kahawa chungu ilmradi aisome na kuifuata kindakindaki resipe husika.

Anasema ili kupata kahawa chungu nzuri na yenye mvuto, ni lazima mfanyabiashara anunue kahawa halisi iliyo na harufu ya kuvutia na kuridhisha.

Anaaeleza kuwa upekee wa maandalizi yake ya kahawa chungu unajumuisha kuchanganya kahawa na viungo mbalimbali vilivyosagwa vizuri, ikiwemo tangawizi, mdalasini, iliki na karafuu ambavyo vyote ni vyenye manufaa tele kwa afya ya mnywaji.

Bw Farid anasema yeye pia hutumbukiza sukari, japo kwa mbali, hali inayoifanya kahawa chungu yake kuwa mwiroro hata zaidi.

“Wengi wanakosa kuelewa maana ya kahawa chungu. Wanadhani wakikoroga tu unga wa kahawa kwenye maji eti kazi imeisha. Hiyo si kahawa chungu. Mimi nimehakikisha ninakoroga unga wa kutosha wa kahawa. Naweka viambata kama vile mdalasini, karafuu, iliki, na pilipili manga kumvutia, kumnasa na kumweka mteja wangu. Ndio sababu wanaoonja kahawa chungu yangu huwa hawataki kwenda kwingine,” akasema Bw Farid.

Yeye huuza vikombe vyake vya kahawa chungu kwa kati ya Sh15 na Sh40 kulingana na ukubwa wa vikombe hivyo.

Bw Farid Mohamed Silaha,62, almaarufu Farid Kahawa akiosha kikombe kabla ya kumtilia mteja kahawa. Yeye ni mweledi katika kuunda kahawa chungu, akidumu kwenye biashara hiyo kwa karibu miaka 25 sasa. PICHA | KALUME KAZUNGU

Zamani, Bw Farid alisema aliuza vikombe vya kahawa chungu kwa bei ya kati ya Sh3 na Sh5 pekee.

“Mimi niko hapa kisiwani Lamu lakini utashangaa nikikwambia kuwa mapishi yangu ya kipekee ya kahawa chungu yamevutia wateja ndani na nje ya Kenya. Mimi hupata wateja wanaozuru Lamu kujivinjaeri kwa kahawa chungu yangu kutoka Nairobi, Kisumu, Mombasa, Kilifi, Malindi na Lamu. Pia hupata wateja wa mataifa ya nje kama vile Uganda, Tanzania, na ng’ambo, ikiwemo Norway, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani nakadhalika. Wote hawa wakizuru Lamu lazima waulize huyu Farid Kahawa yuko wapi ili wafike kubugia kahawa chungu yangu,” akasema Bw Farid.

Bw Farid alizaliwa kijiji cha Matondoni kisiwani Lamu mnamo 1961.

Alisomea shule ya msingi ya Matondoni kabla kuhihitu elimu yake ya darasa la saba kwa wakati huo.

Hakuweza kusonga mbele kimasomo kwa sababu ya uchochole katika familia yake.

Yeye ni mzawa wa saba katika familia ya watoto wanane.

Ana mke na ni baba wa watoto watatu.

Anasema biashara yake imemwezesha kuikimu vyema familia yake mbali na kuwalipia karo watoto wake watatu.

“Nimefaulu kuwasomesha wanangu. Siwezi kuiacha biashara hii kamwe. Nimeipenda kwa moyo wangu wote. Kipendacho moyo dawa,” akasema Bw Farid.

Je, alipata wapi ujuzi wa kupika kahawa ya kuvutia?

Bw Farid Mohamed Silaha,62, almaarufu Farid Kahawa akiwa eneo lake la biashara kisiwani Lamu. Yeye ni mweledi katika kuunda kahawa chungu, akidumu kwenye biashara hiyo kwa karibu miaka 25 sasa. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Farid anasema yeye hakukaa darasani kusomea taaluma hiyo.

Anasema alitumia muda mwingi kutazama waliokuwa weledi wa kuandaa kahawa chungu kijijini kwao Matondoni.

“Kila nikifuatilia kwa karibu waliotengeneza kahawa chungu, baadaye niliyafanyia mazoezi yale niliyoyaona au kushuhudia. Nashukuru kwamba mwishowe niliibukia kuwa gwiji katika nyanja hii,” akasema Bw Farid.

Baadhi ya wateja waliohojiwa na Taifa Leo walimsifu mzee Farid kutokana na ufundi wake katika kuiunda kahawa chungu, hali inayoendelea kumtofautisha na wengine mfano wa ardhi na mbingu.

Ahmed Omar anasema anapotoka kazini kila siku nyakati za jioni, ni lazima apitie kwa mzee Farid kwanza kubugia kahawa chungu kabla ya kuelekea nyumbani kwake kutana na mkewe, familia na jamaa kwa ujumla.

Anasema kahawa chungu humuondolea uchovu wa siku na msongo wa mawazo unaochangiwa na pilkapilka za mchana kutwa za kusaka riziki.

“Nimefanya kana kwamba ni uraibu wa kunywa kahawa chungu kila jioni ifikapo. Punde nikinywa hii kahawa chungu mavune hutoweka mwilini. Hujihisi mchangamfu wa viungo na akili na kuwa mwenye kuburudika kabisa,” akasema Bw Omar.

Thomas Harry, mtalii kutoka Uingereza anasema yeye binafsi amejenga urafiki na watu wengi kisiwani kupitia hiyo kahawa anayokunywa kwa mzee Farid.

“Hii kahawa chungu inaburudisha na pia husaidia waja kujenga urafiki hasa kila mnapokutana na wengine kujiburudisha kwa kinywaji hiki. Mimi nimeishi Lamu kwa miezi sita sasa na niko na marafiki wengi tunaokunywa kahawa chungu pamoja,” akasema Bw Harry.

Bi Fatma Athman anataja kahawa chungu kuwa kinywaji kinachotumika sana, hasa katika nyumba nyingi za Waswahili wa Pwani ya Kenya kukaribishia wageni nyumbani.

Baadhi ya tafiti zilizofanywa zilionyesha miongoni mwa faida kubwa za unywaji wa kahawa kwa mnywaji ni kupunguza hatari ya kupata magonjwa ya ini na saratani.

Pia hupunguza kiwango cha klupata kiharusi japo watafiti bado hawajaweza kuthibitisha kuwa kahawa ndio sababu ya upungufu wa athari hizo.

  • Tags

You can share this post!

Lojing’i ya Nakuru ambayo haina walevi wala makahaba

Mwalimu anayetembea na risasi mguuni kwa miaka 8

T L