• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 9:50 AM
Mwalimu anayetembea na risasi mguuni kwa miaka 8

Mwalimu anayetembea na risasi mguuni kwa miaka 8

NA KASSIM ADINASI

SHAMBULIO la kigaidi la Aprili 2, 2015, katika Chuo Kikuu cha Garissa lilisababisha kiwingu cha huzuni baada ya watu 148 kupoteza maisha naye Mwalimu James Odongo akiachwa na majeraha baada ya kupigwa risasi mara tatu.

Mwalimu huyo ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 48 ni baba wa watoto watano na majuzi alimpoteza mke wake.

Bw Odongo anatembea risasi ikiwa kwa mguu wake wa kulia. Amekuwa akivumilia uchungu huo kwa takriban miaka minane.

Mzaliwa wa Siaya, Bw Odongo alisomea ualimu na kufuzu kufundisha katika shule za msingi na alikuwa katika Chuo Kikuu cha Garissa kujiimarisha kielimu.

“Ninahisi maumivu makubwa na ningependa sana risasi iondolewe mguuni mwangu. Ni uchungu ambao nimevumilia kwa miaka minane,” anasema Bw Odongo.

Alipojeruhiwa wakati wa shambulio hilo, alisafirishwa kwa ndege na akalazwa katika Hospitali ya Kijabe ambapo risasi mbili ziliondolewa ikabaki moja.

Madaktari walimwambia hawangejaribu kuhatarisha maisha yake kutoa risasi hiyo moja wakati huo kwa sababu alikuwa akifuja damu nyingi.

Anafaa afanyiwe upasuaji Septemba 11 katika hospitali hiyo ya Kijabe baada ya shughuli hiyo iliyofaa kufanyika Agosti 15, 2023 kuahirishwa alipokosa kupata pesa zilizohitajika kwa matibabu hayo.

“Ili nifanyiwe upasuaji, ninafaa niwe na angalau Sh500,000. Sina kazi yoyote sasa hivi kwa sababu ya hali yangu ya kiafya,” anasema.

Ana bima ya afya inayoweza kumlipia tu Sh300,000 na kiwango kinachobakia ni sharti atoe mwenyewe kwenye mfuko wake.

Aidha, analalamika kwamba serikali imekuwa ikijikokota kuwapa majeruhi fidia.

  • Tags

You can share this post!

Kuandaa kahawa ya kupendwa na wateja si...

Maumivu Tanzania bei ya mafuta ikipaa na kupita ya Kenya

T L