• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Mafuriko: Familia kadha Kisumu zaachwa bila makao, maafa yakiripotiwa   

Mafuriko: Familia kadha Kisumu zaachwa bila makao, maafa yakiripotiwa  

Na MERCY KOSKEI

FAMLIA kadha kutoka Nyando na Nyakach Kaunti ya Kisumu zimefurushwa kutoka kwa makazi yao kufuatia mvua kubwa iliyonyesha siku ya Jumamosi usiku.

Inasemekana kuwa mto Nyando ulipasua kingo zake na kusababisha nyumba kadha kuzama na kuacha familia zilizoathirika kwenye baridi.

Nyumba za kibiashara pia hazikusazwa, huku mali ya thamani isiyojulikana ikisombwa na maji.

Mafuriko hayo pia yaliharibu daraja la Nyando, hivyo kuwa vigumu kwa madereva kupita barabara.

Maafa yaliripotiwa katika kaunti ndogo ya Nyakach, Kisumu East, Muhoroni na Seme huku zaidi ya familia 1, 200 zikiathirika.

Wiki iliyopita Gavana wa Kisumu Prof Anyang’ Nyong’o alitoa msaada wa chakula na bidhaa zingine kwa familia zilizoathirika na mafuriko.

Kupitia taarifa, Prof Nyong’o alisema kuwa serikali ya kaunti inashirikiana na washirika wengine hasa Shirika la Msalaba Mwekundu, UNICEF, SWAP, na World Vision kuhakikisha familia zilizohathirika zimehamishiwa mahala salama.

“Kutokana na mkaasa huu, ningependa kuomba wasamaria wema, kampuni, mashirika yasiyo ya kiserikali, na makanisa mbalimbali  wajitokeze kuchangia vyakula na bidhaa zingine zinazohitajika ili ziweze kusaidia familia zilizoathirika,” alisema Gavana

Kwa sasa wahanga hao wanahitaji chakula, maji na malazi.

Hata hivyo, wakazi wameombwa kuhamia mahali salama ili kuepuka maafa zaidi ya mafuriko.

Gavana alibaini kuwa kwa sasa Idara ya Kupambana na Majanga ya Kaunti imekuwa ikifanya mkutano ili kupitisha mikakati kukabiliana na mafuriko.

“Leo tumeamka na taarifa za kusikitisha kwamba mafuriko yamezidi kuwa mbaya kufuatia mvua kubwa iliyonyesha Jumamosi usiku. Nyumba nyingi ziliharibika na mimea pia kusombwa. Watoto, wazee na watu wanaoishi na ulemavu wameathirika pakubwa,” alisema Gavana.

 

  • Tags

You can share this post!

Atwoli amtaka Raila kusitisha maandamano

Upasuaji wa miili 10 ya wahanga Shakahola waonyesha...

T L