• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:07 PM
Atwoli amtaka Raila kusitisha maandamano

Atwoli amtaka Raila kusitisha maandamano

Na TITUS OMINDE

KATIBU mkuu Muungano wa Wafanyikazi Nchini (COTU) Francis Atwoli amemtaka kiongozi wa upinzani Raila Odinga kudumisha amani huku akisema hana uwezo wa kupatanisha Rais William Ruto na kinara huyo.

Bw Atwoli alimtaka Ruto kumtafuta Odinga ili wapatane kwa ajili ya umoja wa kitaifa.

Akihutubu wakati wa maadhimisho ya Leba Dei 2023, Atwoli alikejeli upinzani kwa kusema kuwa maandamano hayatabadilisha chochote huku akiwataka wanasiasa husika kukumbatia maridhiano na msamaha.

“Lazima tukubali Ruto ndiye rais wa Kenya hata mimi nilikuwa nimesema atajinyonga lakini sijajua silaha ambazo ulikuwa umejihami nazo. Mambo ya Mungu huwezi ukapingana nayo,” alisema Atwoli huku akilinganisha Bw Ruto na wachawi wa kutoka Magharibi mwa nchi.

Hata hivyo, alikiri kuwa hana uwezo kupatanisha wawili hao.

Bw Atwoli alimtaka Rais Ruto kutafuta mbinu bora ya kupatana na kiongozi wa upinzani huku akionya dhidi ya kudhulumu Bw Odinga.

“Mimi sina uwezo wa kushauri Bw Odinga na Rais Ruto ila kuna watu ambao wana ujasiri na uwezo wa kupatanisha wawili hao,” alisema.

Alisema wakati huu jambo la maana kwa viongozi wote ni kusahau yaliyopita na kujiunga pamoja ili kutafuta amani na umoja wa Wakenya wote kwa ajili ya hatima ya nchi.

Kiongozi huyo alikosoa upinzani dhidi ya kushiriki maandamano.

Alitaka viongozi kuweka kila mkakati kuzuia umwagikaji wa damu, akisema asingetaka taka taswira ya Sudan kushuhudiwa nchini.

“Maandamano si suluhu kwa umoja wa nchi singependa Kenya ifikie mahali Sudan imefikia, naomba Wanasiasa wasahau tafauti zao kwa ajili ya umoja wa nchi,” aliongeza Bw Atwoli.

Akitilia mkazo umuhimu wa Rais Ruto kupatana na wapinzani wake, Atwoli alisema ili kujiepusha na maandamano Ruto anapaswa kufahamu tofauti kati yake na wapinzani kwa ajili ya ustawi wa nchi.

“Singepenada tuwe kama Sudan ilivyo kwa saa hii. Tutafute namna ya kushirikiana kwa ajili ya taifa hili,” aliongeza Bw Atwoli.

  • Tags

You can share this post!

Leba Dei 2023: Viongozi wengi wa kisiasa Pwani wakosa...

Mafuriko: Familia kadha Kisumu zaachwa bila makao, maafa...

T L