• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Mama aponda wanawe kwa shoka na kutoweka

Mama aponda wanawe kwa shoka na kutoweka

NA MWANGI MUIRURI

MWANAMKE ambaye inadaiwa aliwashambulia wanawe wawili kwa shoka kichwani katika Kaunti ya Murang’a mnamo Desemba 23, 2023, alikuwa amelalamika kulemewa na maisha kutokana na gharama za juu.

Hatimaye, mama huyo baada ya kuaminika kutekeleza shambulizi hilo lililowaacha watoto hao wa kiume wa miaka miwili na mitano na kuwaacha katika hali mahututi, alitoweka.

Licha ya Rais William Ruto kuwataka Wakenya wawe wazalendo na wasiwe wa kulalamika ovyoovyo, majirani wa mama huyo walisema kwamba alikuwa ameanza kukabiliwa na msongo wa mawazo lakini hawakutarajia mambo yangeishia kuwa janga la aina hiyo.

Maafisa wa polisi walipofika katika boma la mama huyo, waliagiza watoto hao ambao walikuwa hali mahututi wapelekwe hadi katika hospitali ya Kenol na ambapo walihamishiwa hadi katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) kupewa matibabu ya dharura.

Hata hivyo, licha ya majirani kudai kwamba mama huyo alijirusha ndani ya kidimbwi cha maji kilicho katika boma hilo lao, maafisa wa uchunguzi wa makosa ya jinai (DCI) walikifunga.

“Waliwambia kwamba ingekuwa hatari kuingia ndani ya kisima hicho chenye urefu wa futi 50. Walisema watarejea baada ya msimu wa sikukuu kuisha ili iwapo yuko ndani ya kidimbwi hicho, awe ameelea,” akasema Bw David Njau kutoka familia hiyo.

Kwa mujibu wa Naibu Kamishna wa Murang’a Kusini Bw Gitonga Murungi, kisa hicho kiko chini ya uchunguzi wa DCI.

“Ni habari za kutuhuzunisha sana kama wenyeji kwa kuwa mama huyo ambaye kwa sasa ndiye mshukiwa mkuu lakini pia akiwa hajapatikana, alishawishika kwa pepo gani ndipo, kama tuaminivyo, akaamkia kitendo hicho cha kuwashambulia wanawe na kisha akatoweka,” akasema.

Bw Murungi alisema kwamba watoto hao wako katika hali mahututi “lakini ya Mungu hakuna aliye na uwezo wa kuyabashiri kwa uhakika”.

Mbunge maalum Bi Sabina Chege alilia kwamba “huyu shetani wa ghasia anayekita kambi katika Kaunti ya Murang’a anafaa kukemewa ili atuhame na atukome kwa kuwa ametutwika majonzi ya kutosha”.

Bi Sabina alilia kwamba “siku hizi ni kisa baada ya kingine cha ukatili wa mauti Murang’a na hali hiyo inafaa itukome kwa sasa”.

Majirani waliambia Taifa Leo kwamba shaka ya alikokuwa mama huyo ilianza kuingia watu mwendo wa saa tano na ndipo baada ya kutembelea boma lake kuwajulia hali mama huyo na wanaye, wavulana hao wakapatikana ndani ya nyumba wakiwa wamelala sakafuni wakiwa na majeraha ya kupondwa vichwani na shoka likiwa limelala kando yao.

“Taharuki ilitanda na kukaanzishwa msako wa washukiwa na ndipo ilibainika kwamba mama huyo hakuwa nyumbani. Msako zaidi ulitekelezwa na ndipo katika kidimbwi kilichoko karibu na boma hilo kilionekana kikiwa kimetatizwa na ikashukiwa mama alikuwa amejirusha ndani,” akasema Bi Nancy Wangu, jirani.

Alisema kwamba chifu pamoja na wazee wa Nyumba Kumi waliitwa eneo hilo na ndipo baada ya maafisa wa polisi nao kuitwa, uamuzi wa kufunga kidimbwi hicho bila kubaini kama alikuwa ndani uliafikiwa.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Ndindi Nyoro asuta Jubilee kwa kutishia kumng’oa Ruto

Likizo: Walimu wajituma kwa kuuza mayai, kazi za mjengo

T L