• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 PM
Likizo: Walimu wajituma kwa kuuza mayai, kazi za mjengo

Likizo: Walimu wajituma kwa kuuza mayai, kazi za mjengo

NA RICHARD MAOSI

KWA sababu ya hali ngumu ya maisha, baadhi ya walimu wa shule za kibinafsi nchini wanazungusha mayai au kufanya kazi za mjengo mitaani ili kujitafutia kipato cha ziada.

Idadi kubwa ya walimu nchini wanaishi mijini na baadhi waliozungumza na Taifa Leo wamesema zipo changamoto tele kukidhi mahitaji yao yote.

Bi Janet Ngure ambaye ni mwalimu wa Hisabati katika shule moja ya msingi eneo la Rongai, anasema wamiliki wengi wa shule za kibinafsi nchini hawajaongeza mishahara tangu 2020.

Anasema katika historia, ni jambo la kawaida kwa walimu wa shule za kibinafsi kupokea mshahara mdogo, ndiposa akaamua kuchukua hatua ya kuchuuza mayai tangu mwanzoni mwa Desemba 2023.

Aliamua kujitafutia hela za ziada kwa sababu ya ongezeko la makato ya ushuru kwenye mshahara wake.

Mnano 2022. Bi Ngure pia alichukua mkopo wa benki ili kujiongezea masomo kumaanisha ifikapo mwisho wa mwezi, hurudi nyumbani na kati ya Sh4,000 na Sh6,000.

Lakini kupitia biashara ya mayai, anaweza kuunda faida ya kati ya Sh600-800 kila siku.

“Kwa miaka mingi walimu wa shule za kibinafsi wamekuwa wakihama kutoka shule moja hadi nyingine kutafuta maslahi hasa inapofika kila mwanzo wa mwaka,” anasema Bi Ngure.

Mwalimu mwingine, Bw Alphonce Were kutoka eneo la Kinangop katika Kaunti ya Nyandarua, anasema shule za kibinafsi zinachukua wajibu muhimu kukuza sekta ya elimu nchini.

Hata hivyo, hali ngumu ya maisha inafanya walimu kusumbuka kwa sababu waajiri wao wengi wanafanya biashara ya elimu katika mazingira magumu kiuchumi.

“Nyingi ya familia zetu wakati huu wa likizo zinapata mlo mmoja kwa siku kwa sababu ya kupanda kwa bei ya chakula na mahitaji mengine muhimu kama vile kulipa kodi,” asema.

Anasema siku hizi sio walimu wengi ambao huruhusu wanafunzi kupokea masomo ya ziada almaarufu kama tuition.

Ili kuzima changamoto zinazomkabili, Bw Were angalau hufanya kazi ya mjengo mara tatu kwa wiki ili asikwame hasa muda huu anaposubiri shule kufunguliwa mwaka 2024.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya Rais William Ruto kutoa hakikisho kwamba walimu ambao hawana kazi watapatiwa ajira ya kudumu.

Wengi wao wakiwa ni wale wa Sekondari ya Msingi almaarufu Junior Secondary (JSS) ambao wanahofia huenda mkataba wao ukafikia tamati mwisho wa mwaka huu 2023.

  • Tags

You can share this post!

Mama aponda wanawe kwa shoka na kutoweka

Mama aliyejeruhi wanawe aliambia kanisa ‘kuna...

T L