• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:50 AM
Matiang’i atisha kufunga vyombo vya habari vinavyotumika kueneza chuki

Matiang’i atisha kufunga vyombo vya habari vinavyotumika kueneza chuki

Na ERIC MATARA

SERIKALI imetishia kuvifunga vyombo vya habari vinavyotumika kueneza chuki huku kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022 zikishika kasi nchini.

Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i jana alisema kuwa vyombo vya habari, hasa vinavyotumia lugha za kiasili, vimekuwa vikitumika kueneza matamshi yanayolenga kuzua uhasama wa kikabila nchini.

Dkt Matiang’i aliyekuwa akizungumza mjini Ol Kalou, Kaunti ya Nyandarua, alisema kuwa atatumia mamlaka yake kuhakikisha kwamba vituo vinavyotumiwa na wanasiasa kueneza chuki vinafungwa ili kuzuia fujo kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu ujao.

Alijitetea kwamba vituo vinavyoeneza chuki vitafungwa ili kudumisha amani nchini na wala si ishara ya kugandamiza uhuru wa vyombo vya habari.

“Ni jukumu la vyombo vya habari kuwa katika mstari wa mbele kuhubiri amani bila kuegemea mrengo wowote,” akasema Waziri Matiang’i.

Waziri huyo wa Usalama, alitoa onyo hilo huku visa vya wanasiasa kutumia wahuni kukabiliana na wapinzani wao vikionekana kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Naibu wa Rais William Ruto alikuwa kiongozi wa hivi karibuni msafara wake kushambuliwa na wahuni alipokuwa akijipigia debe mjini Busia.

Vijana hao waliofunga barabara kumzuia Dkt Ruto kuingia mjini Busia, walitawanywa na maafisa wa polisi wa kukabiliana na ghasia.

Jana, Dkt Matiang’i alisema kuwa tayari washukiwa wanane wamekamatwa kuhusiana na vurugu hizo.

Alisema washukiwa wengine waliohusika na ghasia hizo wangali wanasakwa na polisi.

“Sisi Wakenya tuliamua kukumbatia demokrasia. Hiyo inamaanisha kwamba tunasikilizana na kufanya kazi pamoja. Kutofautiana kimawazo miongoni mwa viongozi si sababu ya kutosha kusababisha vurugu na utovu wa amani nchini,” akasema Dkt Matiang’i.

You can share this post!

Hofu idadi ya walimu wanaokufa karibu na maeneo ya...

Aina mpya hatari ya corona yagundulika

T L