• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 8:55 PM
Mchezo wa paka na panya ‘kanjo’ wakitekeleza marufuku dhidi ya wachuuzi jijini Nairobi

Mchezo wa paka na panya ‘kanjo’ wakitekeleza marufuku dhidi ya wachuuzi jijini Nairobi

NA WINNIE ONYANDO

MCHEZO wa paka na panya kati ya wafanyabiashara wanaotandaza bidhaa zao nje ya maduka makubwa na kando ya barabara na maafisa wa idara ya ulinzi (kanjo) ulishuhudiwa Alhamisi katikati mwa jiji la Nairobi.

Hali hiyo ilishuhudiwa kufuatia agizo lililotolewa na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja kuwa hataki kuwaona wachuuzi hao wakikatiza shughuli muhimu katikati mwa jiji.

Baadhi ya wafanyabiashara hao waliepuka kutandaza bidhaa yao hasa katika sehemu zilizopigwa marufuku, hatua inayoonyesha kuwa utekelezaji wa agizo hilo unachukua mkondo chanya.

Akizungumza Jumatano baada ya kukutana na maafisa wa idara ya ulinzi, Gavana huyo alisema kuwa hatua hiyo inalenga kuboresha sura ya jiji kama ilivyo kwenye manifesto yake.

“Lazima jiji liwe na utaratibu. Hii ndiyo maana napiga marufuku uuzaji wa bidhaa kwenye veranda na kando ya barabara kuanzia kesho (jana Alhamisi),” akasema gavana Sakaja.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya wachuuzi wa mayai na smokies kufurushwa kimadharau na maafisa wa kanjo, jambo lililomfanya gavana huyo kuwafidia wafanyabiashara hao.

Maafisa hao wa kanjo wamekuwa wakimulikwa kutokana na jinsi wanavyowafurusha wafanyabiashara bila huruma.

Hata hivyo, Bw Sakaja aliwahimiza maafisa hao kutekeleza wajibu wao bila uoga.

Wananchi wamekuwa wakilalamika kutokana na wachuuzi hao wanaojaza barabara na kutatiza shughuli za usafiri.

  • Tags

You can share this post!

Mke amebadilika sana, baridi imetanda chumbani. Nishauri

Jinsi mfanyabiashara alivyojinasua kutoka kwa ‘mchele...

T L