• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Mtaa kwenye mpaka hata polisi waogopa!

Mtaa kwenye mpaka hata polisi waogopa!

Na BENSON AMADALA

MTAA wa Sofia katika Kaunti ya Busia kwenye mpaka wa Kenya-Uganda ambao unaogopwa hata na polisi, ni eneo ambalo limekuwa likitumiwa kila siku na magenge kuingiza bidhaa haramu nchini.

Japo ni mtaa wa mabanda ambao wengi wa wanaoishi ni watu maskini, maafisa wa polisi huwa hawadhubutu kufika na kupambana na magenge yaliyojihami vikali ambayo yanasimamia uingizaji wa bidhaa hizo, mara nyingi wakilazimika kushirikiana nao.

Unapowasili mtaani humo, shughuli huwa ni nyingi huku wahudumu wa bodaboda wakiendelea na usafirishaji wa bidhaa nao raia kutoka Uganda na Kenya wakivuka mpaka watakavyo huku polisi waliojihami kwa bunduki wakitazama tu bila kuchukua hatua zozote.

Licha ya umaskini huo, biashara ya kuingiza bidhaa kama sukari, mchele, nguo za mitumba, sigara, makaa na pombe ya bei rahisi huwa imekolea. Katika umaskini huo huo, wengi wa wenyeji wa mtaa huo ni waraibu wa matumizi ya dawa za kulevya.

Kutokana na shughuli hizo, wafanyabiashara wanaohusika ambao hudhamini magenge katika mtaa huo, hunufaika pakubwa. Kwa mfano, gunia ya kilo 50 ya sukari huuzwa Sh4,000 Uganda ila likipitishwa na kuingizwa nchini, bei hiyo hupanda hadi Sh6,000.

Kando na wahudumu wa bodaboda, watoto na watu wazima ambao hujifanya ni walemavu wamekuwa wakitumiwa kuingiza bidhaa hizo nchini. Pia magari ya uchukuzi aina ya Probox pia hutumika na wafanyabiashara wanaohusika na ukora huo kusafirisha sukari na bidhaa nyingine ghushi.

Mwandishi huyo alipozuru mpaka huo, alitambua kuwa polisi hawana jingine ila kushirikiana na wahudumu wa bodaboda ambao huendesha pikipiki hizo kwa kasi mno.Wahudumu hao wanafahamiana na polisi hao na huruhusiwa kuondoka na bidhaa hizo ghushi.

Upande wa Uganda, kuna baa ambayo imetengenezwa kwa mbao ambapo pombe ya kitamaduni hutengezwa, ikiwa kitovu cha sherehe mpakani.Wateja humiminika kwenye baa hiyo wakinywa pombe na kushangilia huku pombe hiyo inayofahamika kama enguli ambayo ni sawa na chang’aa ikiwapa msisimko.

Upande wa Kenya nao kuna mtaa wa mabanda mwingine ambao huitwa Marachi. Shughuli za wageni hufuatiliwa sana na baadhi ya wafanyabiashara ambao huwa wameketi sehemu maalum, baadhi wakibadilisha pesa mpakani na wengine wakishirikiana na polisi kuingiza bidhaa ghushi.

Aidha, ni mtaa ambao kujitambulisha kama mwanahabari au anayechunguza suala fulani huwa ni hatari japo ukiomba msaada wa kupitisha bidhaa zako mpakani lazima ‘uchote’ kidogo kwa polisi na magenge hayo. Kuwafichua au kubishana nao ni kama kusaka tiketi ya kifo.

Kutokana na kushamiri kwa biashara haramu hasa ya kuingiza sukari, wakulima wa miwa wamewashutumu polisi kwa kushirikiana na magenge hayo huku wakinufaika na mamilioni ya pesa. Vituo vingine vinavyotumika kuingiza sukari hizo ni Alupe, Busitami na Soko Matope.

You can share this post!

PAA kuhudhuria mkutano wa Raila Kasarani

Wahadhiri, wahudumu wa vyuo vikuu vya umma watishia kugoma

T L