• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Mtandao wa bure wazinduliwa katika masoko ya Pwani

Mtandao wa bure wazinduliwa katika masoko ya Pwani

NA FARHIYA HUSSEIN

SERIKALI kuu imezindua rasmi kwa mara ya kwanza mtandao wa bure katika Soko ya MacKinnon Kaunti ya Mombasa, katika msururu wa mpango wa Rais William Ruto wa kuwekeza katika mawimbi ya mawasiliano kwenye soko mbalimbali.

Wafanyabiashara hao sasa huenda wakapata afueni kuwezeshwa kutumia mtandao wa kijamii, kujiendeleza kibiashara.

Kulingana na Waziri wa Teknoljia ya Habari na Mawasiliano Bw Eliud Owalo, serikali ina mipango ya kuwekeza maeneo 25000 ya mawasiliano hayo ya bure katika masoko mbalimbali humu nchini.

“Wafanyabiashara walilamika wakati wa kampeni wakasema wanataka mawasiliano ya bure kutoka kwa serikali. Tumeanza kwa kuwekeza kwenye masoko kisha tuzindue nyingine kwenye vituo vya kuabiri gari,” akasema Bw Owalo.

Waziri huyo alieleza kuwa mpango huo, unalenga kuwasaidia wafanyabiashara kujiendeleza.

“Dunia imebadilika, si lazima muuzaji na mnunuzi wakutane. Mfanyabiashara anaweza kupiga picha bidhaa na kuweka kwenye mtandao akisubiri kuuza,”’ alisema Bw Owalo.

Aliongezea kuwa serikali itatoa mafunzo ya kidijitali kwa wananchi, ili kuwawezesha kutumia mtandao huo kuwanufaisha.

Naibu Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Bw Ronald Mwiwawi, ambaye alihudhuria uzinduzi huo, aliwahakikishia wafanyabiashara wa soko hilo kuwa, usalama ulikuwa umeimarishwa kuhakikisha wanaendeleza kazi zao kwa urahisi.

“Kamati ya soko inafanya kazi kwa karibu na walinda usalama. Kwenda mbele tunataka masoko yafanye kazi masaa 24. Hii itasaidia kuleta watalii jijini. Si lazima nije sokoni sasa, naeza agiza kutoka kwa mtandao wa kijamii na niletewe nyumbani,”’ alisema Bw Mwiwawi.

Muuzaji wa matunda Bw Lukas Karisa, alipongeza uzinduzi huo, akisema huenda ukawasaidia ila, akalalamikia ugumu wa gharama ya maisha.

“Nimefuirahi kujua sasa nitakuwa na uwezo wa kupata kuuza bidhaa mtandaoni kwa sababu ya Wi-Fi. Ila nina wasiwasi nitauzaje ilhali gharama ya vitu vimepanda. Nimewezeshwa kuuza ila wanunuzi wamenyongwa kiasi kuwa hawana uwezo wa kununua. Ninaomba serikali iangazie hilo pia,” akaseme Bw Karisa.

Waziri Owalo, alizindua mtandao katika soko hilo na lile la wachonga sanamu wa Akamba eneo la Changamwe, akitarajiwa kufungua vituo vingine katika masoko mengine kaunti ya Kwale.

 

  • Tags

You can share this post!

Waiguru aamua kukabiliana na kero la konokono

Ashangaza kutoa kilemba akiteta Mungu ‘amemuacha’ baada...

T L