• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Mume anayedaiwa kumuua mkewe kwa kuuza mavuno ajisalimisha kituoni

Mume anayedaiwa kumuua mkewe kwa kuuza mavuno ajisalimisha kituoni

NA MWANGI MUIRURI

MWANAMUME katika Kaunti ya Kirinyaga mnamo Jumatatu Julai 3, 2023, alijisalimisha katika kituo cha polisi akikabiliwa na tuhuma za kumuua mkewe. 

Mwanamume huyo kutoka kijiji cha Giconjo kilichoko Kirinyaga ya Kati alisikika akilalamika kwamba mke wake alikuwa ameuza kilo 10 za maharagwe zilizokadiriwa kuwa za thamani ya Sh1,500.

Walikuwa wamevuna maharagwe hayo msimu huu baada ya kuvumilia hali ngumu ya kiangazi cha kukosa mvua kwa misimu mitatu mtawalia.

Inadaiwa kwamba baada ya mshukiwa kutekeleza mauaji hayo, alijisalimisha katika kituo cha polisi cha Kianyaga na kujiripoti kama mshukiwa.

Ripoti ya polisi kuhusu kisa hicho inasema kwamba mshukiwa alipandwa na hasira baada ya kukumbuka jinsi alivyoteseka kulisha familia kupitia kununua bidhaa kwa bei ghali madukani na wakati amejaliwa mavuno, mke akayauza.

Alisema kwamba alikuwa akitaka aelezewe kule maharagwe hayo yaliuzwa ili aende kuchukua lakini mke akakataa katakata kufichua na katika hali ya hasira, mauaji yakatokea.

Majirani walisema kwamba wawili hao wamekuwa wakivurugana mara kwa mara.

Mbunge mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Kiriyaga Bi Njeri Maina aliomboleza mauti hayo akisema hayakufaa kamwe.

“Kama mama Kaunti sijafurahia kamwe tukio hilo kwa kuwa ni la kikatili. Nawasihi sana wote katika kaunti hii yetu tuwe watu wa amani na walio na uwezo wa kutatua mitafaruku kwa njia zinazoimarisha maridhiano wala sio fujo za kusababisha mauti,” akasema.

Bi Maina alisema kwamba “hasira huwa ni hasara” na akawasihi wenyeji wawe wakichukua tahadhari kuu wakati wamejipata katika hali ya makasiriko wasije wakatekeleza ya kujutia baadaye.

Kamishna wa Kirinyaga Bw Nayioma Tobiko alisema kisa hicho ni cha kusikitisha na polisi tayari wamemkamata mshukiwa.

“Mshukiwa yuko katika kituo cha polisi cha Kianyaga huku mwili wa marehemu ukipelekwa katika mochari ya Kirinyaga. Mshukiwa atashtakiwa kwa kutekeleza  mauaji,” akasema.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Wazee wa Agikuyu walivyotafuna pesa za kufidia vijana 2...

Waliohamia kambini kutoroka Al-Shabaab wamzomea kamishna

T L