• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 2:21 PM
Waliohamia kambini kutoroka Al-Shabaab wamzomea kamishna

Waliohamia kambini kutoroka Al-Shabaab wamzomea kamishna

NA KALUME KAZUNGU

WAKIMBIZI wanaoishi kwenye kambi ya Shule ya Msingi ya Juhudi, kaunti ya Lamu wamemzomea kamishna wa eneo hilo Bw Louis Rono kwa kuwataka kurudi vijijini mwao akidai usalama umeboreshwa.

Bw Rono alikuwa ametembelea kambi hiyo, akiwa ameandamana na Inspekta-Jenerali wa Polisi Japhet Koome, ambapo wote waliwahakikishia wakazi kwamba serikali inawalinda.

Zaidi ya familia 60 zimepiga kambi shuleni Juhudi tangu Juni 25, 2023, siku moja baada ya watu watano kuuawa kwa kuchinjwa na nyumba sita kuteketezwa moto na magaidi wanaoaminika kuwa wa kundi la Al-Shabaab kwenye vijiji vya Salama na Juhudi, kaunti ya Lamu.

Magaidi wapatao 60 waliojihami kwa silaha hatari, ikiwemo bunduki, mapanga na visu, walivamia vijiji hivyo majira ya saa moja na nusu usiku, ambapo waliwashurutisha wakazi, hasa wanaume kutoka kwa nyumba zao na kisha kuwafunga kamba miguuni na mikononi kwa nyuma kabla ya kuwaua kwa kuwachinja.

Miongoni mwa waliouawa ni mwanafunzi wa kidato cha tatu wa shule ya upili ya Bakanja, Barrack Hussein,19 ambaye alikuwa amefika nyumbani jioni hiyo kwa likizo fupi ya katikati ya muhula.

Tangu hapo, wakazi wameapa katu hawatabanduka kwenye kambi hiyo ya Shule ya Msingi ya Juhudi hadi pale serikali itakapowajengea kambi za jeshi (KDF) na polisi vijijini mwao.

Bw Rono aidha alijipata pabaya pale alipowasisitizia wakazi kuvunja kambi na kurudi makwao, akishikilia kuwa serikali imefanya kila jitihada kudhibiti usalama kote Lamu.

“Tumefika hapa leo pamoja na Inspekta-Jenerali wa Polisi, Japhet Koome ili kuwathibitishia kuwa usalama wenu na mali unadhibitiwa vilivyo. Na hii ndiyo sababu ninashangaa kwa nini mnaendelea kukaa hapa kambini ilhali vijiji vyenu vimelindwa vilivyo. Mrudi mshambani kwenu kuendelea na maisha kwani usalama umedhibitiwa vilivyo kule kuliko hapa kambini mlipo. Kukusanyana hapa kambini ni kuhatarisha tu maisha yenu. Mrudi vijijini,” akasema Bw Rono.

Wakimbizi waliokuwa wakifuatilia hotuba yake walianza kupaza sauti ‘hapana, hapana, hatuwezi, haiwezekani’ kuashiria kwamba hawako tayari kukubali pendekezo la kuvunja kambi na kurudi vijijini.

Bw Peter Muereithi, mmoja wa wakimbizi, alisema wao wataendelea kulala kambini usiku pekee na kurudi makwao mchana.

Bw Mureithi alisema kurudi makwao na kulala huko usiku ni sawa na kujipeleka kichinjioni.

“Hatukubaliani na kaunti kamishna kwamba eti vijiji vyetu ni salama. Eti tunapaswa kurudi huko kuishi usiku na mchana. Huko ni sawa na kujipalia makaa. Magaidi bado wanatafuta mwanya wa kutupata na kutuangamiza. Tutaendelea kulala hapa kambini hadi pale serikali itakapojenga kambi za KDF na polisi vijijini mwetu,” akasema Bw Mureithi.

Bw Titus Mwangi alihoji kwa nini serikali imekuwa ikijitokeza punde wananchi wanapouawa na kupeana ahadi ambazo hazitimizwi.

Bw Mwangi anasema wakazi wamekuwa wakililia kambi za walinda usalama kujengwa vijijini mwao bila mafanikio, mwanya ambao magaidi wamekuwa wakitumia kuvamia vijiji vyao na kuwaua.

“Nakumbuka mwaka jana Januari, watu sita waliuawa kwenye vijiji vya Juhudi, Widho, Mashogoni, Marafa na Ukumbi. Wakuu wa usalama walifika papa hapa kambi ya wakimbizi ya Juhudi kwa wakati huo. Wakaturai kurudi vijijini mwetu wakidai usalama umeboreshwa. Baadaye wakatusahau hadi watu watano wakauawa tena juma lililopita. Saa hii tuko hapa kambini, wakuu wa usalama wamerudi tena wakiturai kurudi kwetu eti usalama umeimarishwa. Hatuwezi kuondoka hapa. Tumechoka na ahadi za uongo za serikali ilhali sisi ndio tunaomalizwa na hawa majangili,” akasema Bw Mwangi.

Bi Mary Achieng kutoka kijiji cha Salama alisema ipo haja ya serikali kuboresha miundomsingi, ikiwemo barabara na hata mawasiliano vijijini mwao ikiwa ingependa wao wavunje kambi na kurudi mashambani.

Kwa mujibu wa Bi Achieng, ukosefu wa barabara na ugumu wa mawasiliano ni vigezo vinavyotumiwa na magaidi kuwavamia kila mara.

“Magaidi wamezoea kuingia vijijini mwetu kutuua na kutawala wakijua fika uchukuzi ni tatizo. Mawasiliano pia ni magumu huku kwani hakuna mawimbi ya kutegemea kuwasiliana na wahusika wakati tuko kwa shida. Twaomba serikali iboreshe haya kabla ya kuturai kurudi vijijini mwetu,” akasema Bi Achieng.

Familia nyingi zinazoishi kwenye kambi ya wakimbizi ya shule ya msingi ya Juhudi ni zile za kutoka vijiji vya Salama, Juhudi, Mashogoni, Ukumbi, Widho, na viungani mwake.

  • Tags

You can share this post!

Mume anayedaiwa kumuua mkewe kwa kuuza mavuno ajisalimisha...

Cherargei aisuta Mahakama kwa kuzima uteuzi wa CASs 50 na...

T L