• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Muuzaji bangi ang’ata na kurarua mdomo wa polisi aliyefika kumkamata

Muuzaji bangi ang’ata na kurarua mdomo wa polisi aliyefika kumkamata

NA MWANGI MUIRURI 

KULIZUKA kizazaa katika mji wa Maragua ulioko katika Kaunti ya Murang’a baada ya mshukiwa wa ulanguzi wa bangi kumuuma afisa wa polisi mdomoni na kurarua kipande cha nyama ya afande hadi kwa kidevu.

Kwa mujibu wa ripoti ambayo iliandikishwa katika kituo cha polisi cha Maragua, mshukiwa huyo inadaiwa alifanya kosa hilo katika mtaa wa Mathare akijaribu kukataa kukamatwa na kutiwa pingu.

“Ni ukweli kwamba kuna mshukiwa wa ulanguzi wa mihadarati ambaye tumekuwa tukimsaka kwa kila aina ya mbinu lakini akituponyoka kila mara tukimwekea mtego,” akasema mkuu wa tarafa ya Maragua Bw Joshua Okello mnamo Desemba 18, 2023.

Alisema alasiri hiyo, afisa mmoja alifika eneo la uuzaji bangi hiyo akijifanya kuwa ni mteja.

“Polisi huyo tuliyekuwa tumemtoa katika kituo jirani ili asifahamike na mshukiwa huyo, aliagiza misokoto mitatu ya bangi kwa gharama ya Sh150 na wakati muuzaji alikuwa anasubiri kulipwa, afisa huyo akachomoa pingu na kumtangazia kwamba alikuwa anatakiwa ashirikiane akamatwe,” Bw Okello akasema.

Hata hivyo, mshukiwa ambaye alikuwa tayari ameshikwa mkono wa kulia na afisa huyo alimjongea afisa kana kwamba alikuwa akitaka kumnong’oneza jambo fulani na akamuuma mdomoni ghafla.

“Polisi amepata majeraha katika upande wa chini wa mdomo wake hadi kwa kidevu lakini katika kisa cha ujasiri mkuu, mshukiwa huyo alishindwa kuponyoka,” akasema Bw Okello.

Bw Okello alisema kwamba afisa huyo alikwamilia mshukiwa huyo licha ya maumivu makali huku maafisa wengine waliokuwa wamevizia katika maeneo tofautitofauti nyanjani wakikimbia kumsaidia mwenzao.

“Hatimaye mshukiwa alitiwa pingu mikononi huku afisa wetu akipelekwa hospitalini kutibiwa. Kwa sasa, mlanguzi huyo yuko kizuizini na atashtakiwa kwa makosa ya kuuza bhangi, kukaidi kukamatwa na kushambulia afisa wa serikali akiwa kazini yake,” akasema Bw Okello.

Naibu Kamishna wa Murang’a Kusini Bw Gitonga Murungi alisema kwamba “visa vya kushambuliwa kwa maafisa wa polisi lazima vizimwe”.

Alipongeza maafisa wake kwa kutekeleza busara ya kujizuia kutumia risasi katika kisa hicho, lakini akawatahadharisha dhidi ya kuwaonyesha washukiwa upole kupindukia.

“Sheria inampa polisi ruhusa kutumia risasi kujinusuru wakati wa uvamizi wa kila aina. Lakini kwa hili tukio, maafisa wetu walidhihirisha utendakazi wa kujitolea kwa kiwango kikuu na kujizuia,” akasema Bw Murungi.

  • Tags

You can share this post!

Zari: Siwezi kurudiana na Diamond ila ni mshikaji wangu sana

Polisi anayetuhumiwa kumjeruhi mzee katika mzozo wa pombe...

T L