• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
Pokot Magharibi waingiwa na hofu visa vya mauaji vikiripotiwa msimu wa Krismasi

Pokot Magharibi waingiwa na hofu visa vya mauaji vikiripotiwa msimu wa Krismasi

NA OSCAR KAKAI

JUHUDI za kusaka amani katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la ufa zimepata pigo huku mauaji na visa vya mashambulio vikiendelea kushuhudiwa msimu huu wa Krismasi.

Mnamo Jumapili usiku, mtu mmoja alipigwa risasi na wengine kujeruhiwa vibaya na majangili huku maelfu ya mifugo ikiibwa katika kijiji cha Ombolion, Kaunti ya Pokot Magharibi.

Wiki mbili zilizopita, watu saba, watatu kati yao wakiwa wakazi kutoka Kaunti ya Pokot Magharibi wanadaiwa kuuawa na maafisa wa usalama wanaondeeleza operesheni ya kiusalama katika eneo hilo, watatu wakiwa washukiwa wa ujangili wanaosemekana kutoka kaunti jirani ya Turkana ambao walipigwa na kuawa  baada ya kuvamia kijiji cha  Lochacha, eneo la  Turkwel.

Naye mtoto mwenye umri wa miaka mitatu aliuawa eneo la Chesegon na majangili wanaoshukiwa kutoka kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Wakazi na viongozi wa eneo hilo wakiongozwa ma mbunge wa Kapenguria Samuel Moroto na naibu spika katika bunge la kaunti ya Pokot Magharibi Victor Sigwat, wamelalamikia kuhusu mauaji na mashambulio ya mara kwa mara kwenye mipaka ya kaunti ya Pokot Magharibi licha ya mchakato wa kutafuta amani kuendelea.

Haya yanajiri baada ya kombe la soka la amani  la Kaskazini mwa Bonde la ufa ambalo lilivutia maelfu ya wakazi kutoka jamii hasimu  za Pokot, Marakwet na  Turkana, mawaziri watatu, magavana watatu, wabunge kumi na watu wengine mashuhuri  kuandaliwa katika mji wa  Kapenguria mnamo Jumapili.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi kutoka kaunti hiyo wamekuwa wakipinga kombe hilo wakisema kuwa ni kejeli na onyesho mbaya wakati mauaji yanaendelea  kushuhudiwa. Baadhi ya viongozi hasa waakilishi wadi ambayo waliandamana siku chache zilizopita kuhusu mauaji walikataa kuhudhuria zoezi.

Walisema kuwa mchakato wa amani kupitia kombe la soka ambalo lilifadhiliwa na waziri wa barabara Kipchumba Murkomen halijazaa matunda sababu mashambulizi bado yanaendelea kushuhudia eneo hilo.

Walisema kuwa kombe hilo liliangazia tu wasomi na watu wa mijini bali sio warani kamili na viongozi kwenye zizi  mashinani.

 Kulingana na Bw Moroto, kombe hilo la amani lingefanyika kwenye maeneo ambayo hushuhudia utovu wa usalama likishirikisha jamii za mashinani na viongozi wote.

“Kombe hilo lingefanyika kwenye maeneo hatari kama Chesegon na Turkwel na warani kupewa kipau mbele. Tunataka misafara ya amani.  Tunataka warani waje na wacheze densi,” alisema Bw Moroto.

Bw Sigwat aliisuta serikali kwa kufeli kulinda wakazi wa kaunti ya Pokot Magharibi.

“Hiyo droni iliorusha grunedi ikaua watu wetu ilikuwa wapi wakati majahili walikuwa wanavamia watu wetu? Wanajeshi ambao wanaishi eneo la Loyapat walikuwa wapi wakati wa shambulio? Wanafaa kuwa chonjo na kushika doria,” alisema Bw Sigwat ambaye pia ni mwakilishi wa wadi ya Endough.

Mwakilishi wa wadi mteule Marishana Cheruto aliitaka serikali kuondoa silaha zote haramu kutoka eneo hilo.

“Hakuna ujahili na hakuna vita mjini Kapenguria. Kombe hilo lilikuwa la starehe,” alisema.

Mkazi Job Lokwakor alisema kuwa wakazi wameuawa kwenye kaunti ilhali serikali haifanyi lolote.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Murkomen motoni kwa kudai Rwanda ni taifa la kidikteta

Mafuriko: Kukatika barabara kwafanya wakazi Lamu kutambua...

T L