• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Murkomen motoni kwa kudai Rwanda ni taifa la kidikteta

Murkomen motoni kwa kudai Rwanda ni taifa la kidikteta

NA CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen amelaumiwa kwa kudai kuwa taifa la Rwanda linaongozwa kidikteta ambapo kile Rais husema huchukuliwa kama sheria.

Akijibu maswali kuhusu masuala ya usalama wa barabara kwenye runinga ya Citizen, Bw Murkomen alieleza kuwa utekelezaji wa maamuzi ya serikali huchukua muda “kwa sababu Kenya ni demokrasia ambako utawala wa sheria huzigatiwa.”

Alikuwa akijibu malalamishi kutoka kwa wananchi kuhusu kucheleweshwa kwa utekelezwa wa kanuni na maamuzi ya usalama barabarani zilizotolewa na wizara yake, kama mafunzo mapya kwa madereva.

Wakenya hao, akiwemo Seneta wa Kisii Richard Onyonka, alitoa mfano wa Rwanda ambako sheria na kanuni za usalama barabara hutekelezwa kwa haraka.

“Rwanda sio kama Kenya. Rwanda ni taifa linaloongozwa kidikteta ambapo agizo la Rais huwa ni sheria,” akasema Jumatatu usiku.

“Kwa kila uamuzi inayofanywa nchini sharti iwe ni pendekezo linalopasa kupelekwa bungeni kisha maoni ya umma yashirikishwe,” Bw Murkomen akaongeza.

Kauli ya waziri huyo ilizua kero mingoni mwa Wakenya kwenye mitandao ya kijamii, akiwemo Wakili Mkuu Ahmednasir Abdullahi, alisema kauli hiyo inaweza kuchochea uhasama kati ya Kenya na Rwanda.

“Waziri Murkomen hafai kushambulia taifa rafiki ambayo haijachokoza Kenya na yamemkosea heshima Rais wa Rwanda Paul Kagame, bila sababu maalum. Hii ni aibu  na inaweza kusababisha mzozo wa diplomasia kati ya nchi hizo mbili,” akasema Bw Abdullah.

“Sharti mawaziri wafundishwe kuhusu wajibu wa afisi zao, haswa kuhusu diplomasia na sheria za kimataifa,” akaongeza jana kupitia mtandao wa kijamii wa X, zamani twitter.

Naye msomi katika taalum ya Mahusiano ya Kimataifa Macharia Munene alisema ni makosa kwa waziri kuipaka tope nchi jirani.

“Wizara ya Masuala ya Kigeni ya Kenya inafaa kutoa taarifa ya kuomba msamaha kwa taifa la Rwanda kuhusiana na madai ya Waziri Murkomen. Hilo lisipofanyika Rwanda itachukuliwa kauli ya Waziri huyo kama iliyoidhinishwa rasmi na serikali ya Kenya, hali ambayo inaweza kuchochea mzozo wa kidiplomasia kati ya nchini hizi mbili,” Profesa Munene akaeleza.

Kwa upande wake, Bw Murkomen amewapuuzilia wanaomsuta kwa kusema kuwa Rwanda inatawaliwa kidikteta.

Waziri alisema anaunga mkono mtindo wa uongozi nchini Rwanda ambao alieleza imeisaidia nchi hiyo “kupiga hatua kubwa kimaendeleo.”

“Rafiki yangu, Ahmednasir, napendezwa na mtindo wa uongozi unaoendelezwa Rwanda ambao umewasaidia kujenga miundo msingi mizuri ukiwemo uwanja mpya wa ndege na kuleta nidhamu barabarani. Sio Rwanda tu, nchi kama vile Umoja wa Milki ya Kiarabu (UAE), Morocco, Saudi Arabia, miongoni mwa nyingi imekumbatia mitindo ya uongozi ambayo ileta ufanikisi kwa sababu viongozi wao wanayo mamlaka ya kufanya maamuzi makali,” Murkome akaeleza.

Mnamo Mei 15, mwaka huu Katibu wa Wizara ya Masuala ya Kigeni Korir Sing’oei alimkaripia Waziri wa Utumishi wa Umma Moses Kuria kwa kutoa kauli tata kuhusu mzozo unaoendelea nchini Sudan.

Bw Kuria alidai kuwa suluhu la kipekee la kukomesha mzozo huo ni kwa wanajeshi wa Umoja wa Afrika (AU) kushambulia Khartoum kwa mabomu.

  • Tags

You can share this post!

Musalia ataka Ruto ashauriane na Museveni kuokoa Wakenya 41...

Pokot Magharibi waingiwa na hofu visa vya mauaji...

T L