• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:55 AM
Seneta Nyutu aitaka Del Monte kukoma kuua vijana Murang’a

Seneta Nyutu aitaka Del Monte kukoma kuua vijana Murang’a

NA MWANGI MUIRURI

SENETA wa Murang’a Joe Nyutu amelalamikia kuongezeka na kuzidi kwa visa vya mabawabu wa kampuni ya Del Monte, iliyoko Kaunti ya Murang’a kuua na kujeruhi majirani.

Kampuni hiyo hushiriki kilimo cha mananasi na kando na kuyauza ng’ambo, huwa inatengeneza juisi.

Seneta Nyutu alisema kwamba mabawabu hao huwasingizia vijana wa kiume walio majirani kwamba ni wezi wa mananasi na huwa wanawapiga hadi kuua baadhi yao, na wengine kuachwa wakiwa na majeraha mabaya.

“Nilimwambia Rais William Ruto kuhusu dhuluma ya kampuni hiyo ya Kimarekani ambayo hudhibiti ekari 30, 000 za shamba miongoni mwa watu wetu alipozuru Murang’a mnamo Julai 21, 2023,” Bw Nyutu akasema.

Bw Nyutu aliteta kuwa kwa miaka mingi kilio kimekuwa kampuni hiyo kufunga barabara ambazo raia wanapaswa kupitia na vijana wa eneo hilo wakiuliza maswali kwa niaba ya wenyeji, wanasingiziwa wizi na hatimaye kutekelezewa unyama.

Bw Nyutu aliteta kuwa “mabawabu hao huwa hawana aibu na huwavamia vijana hao hata wakiwa katika mashamba ya mababu zao wakiendesha shughuli zao halali”.

Bw Nyutu alitoa makataa kampuni hiyo itoe taarifa ya kuhakikishia wenyeji kwamba itakoma ukiukaji wa haki za kibinadamu.

Aidha, aliitaka ijitume kulipa fidia kwa familia ambazo zimeathirika katika kashfa hiyo.

“Kmpuni hii inafaa itekekeze uamuzi wa mahakama ulioitaka itenge ekari 3, 400 za shamba hilo kwa wenyeji,” akasema.

Kampuni hiyo tayari imetoa taarifa ikisema kwamba haki za kibinadamu ni sera yake dhabiti na itashirikiana na wadau wote kuhakikisha hali hiyo imezingatiwa.

Mwito wa Bw Nyutu unawiana na ule wa mbunge wa Gatanga Bw Edward Muriu ambaye wiki jana alilalamika kwamba serikali ya Kaunti ya Murang’a haitilii maanani kilio cha wenyeji kuhusu shamba hilo.

Aidha, Bw Muriu alionya Gavana wa Murang’a Dkt Irungu Kang’ata akome mbio za kutwaa ekari 1, 400 kutoka kampuni hiyo akidai anataka kujenga hospitali na soko.

“Ni uamuzi wa mahakama kwamba kampuni ya Del Monte itenge ekari 3, 400 kwa wenyeji wa Murang’a na zingine 600 kwa wenyeji wa Kaunti ya Kiambu.

“Hapa Murang’a, serikali ya Kaunti inakimbia kutwaa ekari 1, 400 na kusahau kwamba hata haijawahi kushiriki vita vya kupata ugavi huo,” akasema katika mahojiano na kituo cha Televisheni cha Inooro.

Alisema kwamba wakazi wa Kandara na Gatanga ndio wamekuwa wakipigania shamba hilo ligawie wenyeji, huku serikali ya Kaunti ikiwa shabiki tu.

“Katika mbio zake za kuanza kunufaika na matokeo ya vita vya raia, serikali ya kaunti ichunge isituingize kwa shida nyingine hapa. Tushirikishe harakati hizi kwa mpangilio. Ikipata ekari zake za kustawisha kwa miradi ya umma, isisahau kuwa hilo halitawezekana kabla raia wapate ekari zao 2, 000,” akasema.

Bw Muriu alisema kwamba “tunataka shamba la umma litenganishwe na lile la Kaunti. Ekari 2, 000 ziwekwe kando ili wapiga kura wa Gatanga na Kandara wakae chini waamue jinsi watakavyogawana”.

Bw Nyutu pia alisema ni lazima wenyeji wapate shamba lao huku akilalama kwamba serikali ya kaunti ilikimbia kutwaa ekari 1, 400 huku wenyeji wakisalitiwa.

 

[email protected]

 

 

  • Tags

You can share this post!

Ajabu polo akimnyunyizia bawabu mkojo na kuacha kinyesi...

Granton Samboja arudi kwa utangazaji redioni

T L