• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Simanzi waliouawa kinyama wakizikwa

Simanzi waliouawa kinyama wakizikwa

NA KALUME KAZUNGU

SIMANZI iligubika vijiji mbalimbali vya Lamu kwa siku mbili tangu Jumanne waathiriwa 13 waliouawa na wahalifu, ikiwemo washukiwa wa al-Shabaab walipozikwa chini ya ulinzi mkali.

Mazishi hayo yaliandaliwa katika vijiji vya Salama, Widho, Hongwe-Msafuni, Muhamarani, ambapo waombolezaji, wakiwemo viongozi wa kisiasa na wenyeji waliishinikiza serikali kuimarisha usalama vijijini.Baadhi ya waliouawa pia walisafirishwa hadi katika kaunti nyingine za bara kwa mazishi.

Katika kijiji cha Salama kilichoko karibu na Widho, mazishi ya Francis Kamau, 45, ambaye aliuawa pamoja na wanakijiji wengine watano katika uvamizi wa Januari 2, 2022 eneo la Widho alizikwa kwenye hafla iliyoshuhudia waombolezaji wachache waliojitokeza Jumanne mchana.

Akihutubia waombolezaji, diwani wa Mkunumbi inayojumuisha vijiji ambavyo wakazi wamekuwa wakivamiwa, Paul Kimani aliisihi serikali kuanzisha kambi za jeshi na polisi wa kitengo cha RDU, hasa kwenye eneo la Juhudi-Ukumbi alilolitaja kama linalotumiwa mara kwa mara kama njia ya magenge yanayoingia vijijini kuua wakazi na kuharibu mali.

“Ninaiomba serikali iongeze doria za jeshi (KDF) na polisi wa RDU maeneo haya ili kuzuia wahalifu wasipenye kuchoma nyumba za watu na kuua wakazi wasio na hatia. Tunalaani vitendo hivi vya uvamizi na mauaji ya kinyama kwa watu wetu. Lazima hali hii ikomeshwe haraka iwezekanavyo,” akasema Bw Kimani.

Naye mgombea kiti cha useneta wa Lamu kwenye uchaguzi ujao, Francis Mugo, aliwasihi Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang’i na mwenzake wa Ardhi, Farida Karoney, kuzuru Lamu na kuchunguza masuala nyeti yanayosababisha utovu wa usalama eneo hilo, ikiwemo kero ya wapiganaji wa al-Shabaab na pia mizozo ya mashamba.

Katika kijiji cha Msafuni, wadi ya Hongwe, kaunti ya Lamu, mwathiriwa mwingine wa uvamizi wa wahalifu, John Murimi alizikwa chini ya ulinzi mkali wa KDF na polisi.

Kwenye hotuba yake kwa waombolezaji, diwani wa Hongwe, James Komu aliiomba serikali kuteua wanakijiji zaidi na kuwapa mafunzo ili kujiunga na kitengo cha askari wa akiba (NPR).

Kulingana na Bw Komu, licha ya wakazi wengi waliokuwa wakihudumu kama NPR kustaafu,hakuna hatua yoyote imechukuliwa na serikali kuteua maafisa wapya.

Alisema anaamini idadi ya NPR ikiongezwa vijijini itasaidia kukabiliana na kumaliza uhalifu, ikiwemo hao majangili wanaoua wakazi.

“Itakuwa bora uteuzi wa maafisa zaidi wa NPR kufanywa haraka. Wapokezwe mafunzo maalum ya kiusalama na wapewe bunduki za kisasa ili kudhibiti usalama vijijini.Pendekezo langu ni kila kijiji cha Lamu kiwe na angalau maafisa watatu au wanne wa NPR,” akasema Bw Komu.

Katika kijiji cha Muhamarani, mwathiriwa Maina Wanjege ambaye alikuwa miongoni mwa watu sita waliouawa Widho Januari 2 na Kipkoloi Mwaura aliyekuwa miongoni mwa wazee wawili waliouawa na wahalifu eneo la Juhudi/Marafa Januari 9, 2022 pia walizikwa.

Kwenye mazishi hayo, waombolezaji waliiomba serikali kuhakikisha usoroveya wa mashamba unatekelezwa na wakazi kupewa hatimiliki za ardhi.

“Ugaidi upo lakini huenda tatizo la mashamba linatumiwa ili kuwachochea wakazi wa hapa kugawanyikana. Ikiwa serikali itasuluhisha hilo tatizo la mashamba na pia kukabiliana vilivyo na Al-Shabaab,Lamu itakuwa sehemu yenye amani na utulivu wa kudumu,” akasema Bi Mary Wambugu.

Waathiriwa wengine wa uvamizi wa Lamu ambao walizikwa juma hili ni polisi wanne wa kitengo cha GSU waliouawa Januari 7, 2022 pale gari walimokuwa wakisafiria liliporushiwa gruneti na kuunguzwa moto maafisa hao wakiwa ndani katika eneo la Milihoi kwenye barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen.

Shambulio hilo linaaminika kutekelezwa na washukiwa wa kundi la al-Shabaab.

Aidha miili ya maafisa hao wanne ilisafirishwa jijini Nairobi siku hiyo hiyo ya shambulio na kukabidhiwa familia zao kwa mazishi.

Wakati wa ziara yake kwenye shule ya kibinafsi ya Shalom Academy iliyoko mjini Kibaoni, ambako familia zaidi ya 100 zimepiga kambi kufuatia utovu wa usalama, mauaji na taharuki vijijini, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia aliwahakikishia wakimbizi hao usalama wao.

“Watu wasiwe na hofu.Tumesambaza maafisa wa kutosha wa usalama vijijini ili kupambana na wahuni ambao wamekuwa wakivamia na kuua wananchi na kuchoma nyumba Lamu,” akasema Bw Macharia.

You can share this post!

Pigo kwa taaluma ya Kiswahili mtaalam akifariki

Serikali yaridhishwa na miradi yake Pwani

T L