• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Ukeketaji Pokot Magharibi unavyochangia kina mama kufukuzwa kwenye boma

Ukeketaji Pokot Magharibi unavyochangia kina mama kufukuzwa kwenye boma

NA OSCAR KAKAI

MILA POTOVU za ukeketaji zimetajwa kuchangia visa vingi vya dhuluma za kijinsia na vurugu katika familia maeneo ya jamii za wafugaji.

Ukeketaji ambao ni aina ya dhuluma za kijinsia huathiri wasichana  na akina mama ambao hukeketwa na kuathirika kiakili ikiwa ni pamoja na kuchangia msongo wa mawazo.

Wasichana wengi, kwa mfano katika Kaunti ya Pokot Magharibi wamepitia ukeketaji ambapo sehemu za siri huondolewa kwa sababu ambazo hazina msingi wowote kimatibabu.

Imebainika kuwa, visa vya ukeketaji, ndoa na mimba za mapema bado vimeshamiri Pokot Magharibi hasa wakati huu msimu wa sherehe za Krismasi zinabisha hodi na likizo ndefu .

Kulingana na shirika la Pokot Outreach Ministries (POM), karibu wasichana 14 kutoka eneo la Kaunti Ndogo ya Pokot Kaskazini  walikeketwa na kutorokea nchi jirani ya  Uganda.

Duru zinaarifu, wanne katika eneo la Sook walikeketwa Oktoba 2023.

Zaidi ya vijana 300 katika wadi ya  Kodich, Kaunti Ndogo ya Pokot Kaskazini walifuzu baada ya kupewa mafunzo kuhusu mbinu mbadala za kupitia shirika la POM.

Mkazi wa Kodich, Charity Chebet alisema kuwa ukeketaji huchangia dhuluma kwa familia ambapo wanaume ambao hulipa mahari nyingi hutaka kuwakeketa wasichana lakini wanawake wanapinga.

“Wakati msichana anatoroka, mama anafukuzwa kuenda kumtafuta,” alisikitika.

Florence Mondi, afisa wa mpango kuinua akina mama katika shirika la POM alisema kuwa ukeketaji unalenga kuharibu sehemu ya siri ya mwanamke.

Seneta wa Pokot Magharibi Julius Murgor ambaye ni mwasisi wa POM alisema kuwa ukeketaji una athari nyingi, ambapo baada ya msichana kukeketwa hutoroshwa na wanaume kwa nguvu.

Alisema kuwa mila hiyo potovu ni hatari kwa akina mama wakati wa kujifungua.

“Baada ya kukeketwa, sehemu ya siri huwa kidogo na kuwa na ugumu mtoto kutoka wakati wa kujifungua. Wasichana wengi huumia sababu  ya makovu ambayo ni nadra kupona.Wanaume huwa na hasira hutokana na ng’ombe nyingi ambao wao hutoa kama mahari,” alisema.

  • Tags

You can share this post!

Kenya Power yakashifiwa kwa utepetevu stima zikipotea kwa...

Vitabu vya mitihani ya KCPE vyaendelea kuuzwa licha ya...

T L