• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Vitabu vya mitihani ya KCPE vyaendelea kuuzwa licha ya mfumo wa 8-4-4 kuondolewa 

Vitabu vya mitihani ya KCPE vyaendelea kuuzwa licha ya mfumo wa 8-4-4 kuondolewa 

NA RICHARD MAOSI 

LICHA ya kukamilika kwa mfumo wa masomo wa 8 – 4 – 4, baadhi ya matapeli jijini Nairobi bado wanauza vitabu vya marudio ya Mitihani ya Kitaifa ya Darasa la Nane (KCPE). 

Ni jambo linalowafanya wazazi wengi kukosa mwelekeo ufaao jinsi ya kutofautisha mfumo mpya wa elimu na ule wa zamani.

Ikumbukwe mtaala wa CBC, yaani mfumo wa 2-6-3-3-3, ulianzishwa 2017 kuchukua nafasi ya 8-4-4, chini ya uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta ambaye kwa sasa ni mstaafu.

Sehemu ambazo zinaendesha biashara yenyewe ni River Road katikati mwa jiji la Nairobi, ambapo kila aina ya bidhaa huuzwa, kutokana na idadi kubwa ya wateja wanaoamini soko hilo la bidhaa za bei nafuu.

Taifa Leo Dijitali imebaini hii ni akiba ya mtaji wa mauzo ya mwaka uliopita, 2022, na wafanyibiashara wengi hawapo tayari kupata hasara.

Alice Yegon mzazi katika shule moja eneo la Syokimau, Kaunti ya Machakos anasikitika soko la sekta ya elimu kusheheni na kujaa vitabu bandia.

Hata hivyo, anawalaumu baadhi ya wazazi kwa kutotilia maanani masomo ya watoto wao.

“Kwanza wanatakiwa kuwa na utamaduni wa kushirikisha wataalam wa elimu ili kufahamu orodha ya vitabu vinavyohitajika shuleni,” akasema wakati wa mahojiano.

Isitoshe, Bi yegon amewataka wazazi hasa wenye watoto katika shule za umma mitaani kuchunguza masomo ambayo yanatahiniwa katika mtaala wa CBC.

Hili linajiri karibu mwezi mmoja tangu waziri wa elimu Ezekiel Machogu kutangaza matokeo ya KCPE 2023 kwa mara ya mwisho tangu mfumo wa 8 – 4 – 4 uanzishwe 1985.

Katika hotuba yake, Waziri Machogu aliambia Wakenya 2023 ni mwaka wa mwisho kupokea matokea ya KCPE baada ya kupisha mtaala wa CBC.

Mwaka huu, 2023, watahiniwa wa kwanza wa gredi ya 6 walifanya mtihani wa KPSEA ili kujiunga na Sekondari Msingi.

 

 

 

 

  • Tags

You can share this post!

Ukeketaji Pokot Magharibi unavyochangia kina mama kufukuzwa...

Tabia za wizi msimu wa Krismasi zilivyomshushia kifungo cha...

T L