• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 12:18 PM
Kenya Power yakashifiwa kwa utepetevu stima zikipotea kwa mara ya tatu maeneo mengi nchini

Kenya Power yakashifiwa kwa utepetevu stima zikipotea kwa mara ya tatu maeneo mengi nchini

NA SAMMY WAWERU

MAENEO mengi ya nchi Jumapili, Desemba 10, 2023 yalikosa nguvu za umeme kwa karibu saa nne mfululizo Wakenya wakikashifu vikali kampuni ya usambazaji stima, Kenya Power.

Nguvu za umeme zilipotea majira ya mbili za jioni, shirika hilo kupitia taarifa likisema tatizo hilo lilitokana na hitilafu ya kimitambo.

Sehemu zilizoathirika ni pamoja na Kisumu, Mombasa, Saba Saba, Bomet, Tana River, Nanyuki, Kakamega, Lamu, Murang’a, Nakuru, Makueni, Tharaka-Nithi, na Machakos.

“Tumepoteza nguvu za umeme maeneo kadha nchini, kwa kile tunachoshuku ni dosari ya kimitambo,” taarifa ya Kenya Power ikaelezea.

Ikaongeza, “Tunafanya kila tuwezalo kurejesha stima. Tutaarifu taifa tukiangazia tatizo hilo. Tunaomba radhi kwa wateja wetu.”

Cha kushangaza, hata afisi za Kenya Power Kisumu zilikosa stima jambo lililoibua maswali kuhusu utendakazi wa kampuni hiyo.

Jumapili jioni, Desemba 10, 2023 maeneo kadha nchini yalisalia giza baada ya stima kupotea. PICHA|SAMMY WAWERU

Tatizo hilo pia liliathiri huduma za treni ya kisasa, SGR, kati ya sekta zingine za dharura zinazotegemea stima.

Aidha, zilirejea mwendo was aa nne usiku.

Nguvu za umeme kupotea Jumapili, Desemba 10, ilikuwa mara ya tatu jambo ambalo linaibua maswali kuhusu utendakazi wa Kenya Power.

Miezi michache iliyopita, hali kama hiyo pia ilishuhudiwa ambapo iliathiri utendakazi katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA), Nairobi na uliochochea baadhi ya wasimamizi kufutwa kazi.

Baadaye, taifa lilijipata katika kitendawili hicho – nguvu za umeme kupotea.

Ni suala ambalo Wakenya wameelekeza ghadhabu zao mitandaoni wakikashifu Kenya Power, wakimtaka Rais William Ruto kufanya mabadiliko katika sekta ya kawi nchini.

Isitoshe, wanalalamikia utepetevu wa kampuni hiyo ya kipekee kusambaza nguvu za umeme.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Huenda mabwanyenye waliotekwa na Kang’ata ni njama...

Ukeketaji Pokot Magharibi unavyochangia kina mama kufukuzwa...

T L