• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 7:55 PM
Wageni wataabika kupata vyumba vya kulala kipindi kizima cha tamasha za utamaduni Lamu

Wageni wataabika kupata vyumba vya kulala kipindi kizima cha tamasha za utamaduni Lamu

NA KALUME KAZUNGU

UHABA mkubwa wa vyumba vya kulala unashuhudiwa kisiwani Lamu wakati ambapo makala ya 21 ya Tamasha za Utamaduni wa Lamu yanafikia ukingoni.

Tamasha hizo za siku tatu zimekuwa zikiendelea tangu Alhamisi na sherehe hizo zinatarajiwa kukamilika Jumamosi usiku.

Zaidi ya wageni na watalii 30,000 wamekongamana kwenye mji huo wa kale wa Lamu kwa maadhimisho hayo ya utamaduni.

Hafla ya utamaduni wa Lamu huadhimishwa kila mwaka kisiwani Lamu, lengo kuu likiwa ni kuzitambua na kujivunia mila na desturi za jamii ya Lamu ambayo ni ya Waswahili wa asili ya Wabajuni.

Aidha tangu sherehe hizo kung’oa nanga, wenye hoteli, mikahawa na gesti wamekuwa wakivuna pakubwa kibiashara kutokana na wingi wa wateja waliofurika visiwani Lamu na Shella kuadhimisha sherehe hizo.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo ulibaini kuwa bei ya vyumba vya kulala imeongezeka, ambapo chumba kilichokuwa kikikodiwa kwa kati ya Sh1,000 na Sh1,500 kwa usiku mmoja, kwa sasa kinakodiwa kwa kati ya Sh3,000 na Sh4,000 kwa kila usiku mmoja.

Licha ya ongezeko la kodi, vyumba vyote vya hoteli na gesti mjini Lamu, Shella na viunga vyake kufikia Alhamisi jioni tayari vilikiwa vimefurika wageni na watalii huku wale waliofika Ijumaa wakikosa mahali pa kulala.

Kuna walioafikia kutumia fedha nyingi zaidi kuvuka miji ya nje ya kisiwa cha Lamu,ikiwemo Mokowe, Hindi, na Mpeketoni kutafuta mahali pa kukodi kulala ilmradi warauke kisiwani Lamu kuhudhuria tamasha kila siku.

Bw Solomon Odhiambo, ambaye ni mtalii wa ndani kwa ndani kutoka eneo la Nyanza anasema alifika kisiwani Lamu na familia yake Ijumaa asubuhi lakini baada ya kuzurura kila mahali kutafuta pa kukodi kisiwani, aliafikia kuvuka Mokowe ambapo alipata hoteli ya kulala na familia.

“Nilikuwa nasikia tu sifa za Lamu mitandaoni,magazetini,maredioni na kwenye televisheni. Baada ya wanangu kufunga shule, nikaamua kuwachukua Na mke wangu tuje Lamu hasa msimu huu wa Tamasha ya Utamaduni ili tujivinjari na kujionea ya hapa. Tumefurahi. Watu Ni wengi. Vyumba vya kulala Ni ghali na hata haipatikani kwa sasa. Ndiposa nimeamua kukodi hoteli Mokowe. Huwa twaja Lamu alfajiiri kila siku kujivinjari na kisha kuvuka tena Mokowe kulala. Tutafanya hivi hadi pale hafla itakapotamatika. Ni raha tupu hapa kisiwani,” akasema Bw Odhiambo.

Bi Isla Jack, mtalii kutoka nchini Uingereza, hakuficha furaha yake baada ya kuhudhuria tamasha za utamaduni wa Lamu kwa mara ya kwanza.

Bi Jack alisema kilichomvutia zaidi msimu huu wa sherehe za utamaduni wa Lamu ni ukarimu na makaribisho sufufu yanayoonyeshwa na wenyeji wa Lamu.

Pia alivutiwa sana na maonyesho mbalimbali ya kitamaduni,hasa ngoma za asili ya eneo hilo kama vile Goma La Lamu, Goma la Pate,Vugo, Goma La Barani,Uta, Kirumbizi na mengineyo mengi.

“Nimevutuwa sana na mbio za punda, mashindano ya jahazi, soka ya ufukweni na mapishi. Lamu kweli ni tamu kwani ina vyakula mwororo kama vile biriani, mkate wa kutetema,mkate wa kupaka, pweza, samaki wa kupaka na pilau. Nimeonja vyakula hivyo vyote na nimebambika. Kweli ziara yangu hapa tamashani si bure,” akasema Bi Jack.

Kutokana na idadi kubwa ya wageni na watalii wanaoendelea kufurika kisiwani Lamu,baadhi ya wenyeji wamezigeuza nyumba zao kuwa maeneo ya wageni kukodi kulala ilmradi pia wafaidi hela nyingi zilizofikishwa kisiwani na waliohudhuria tamasha.

“Ama kweli mgeni njoo, mwenyeji apone. Nilipoona wageni wakihangaika Kwa kukosa pa kulala,fikra ilinijia akilini kwamba Niko Na nyumba kubwa ambayo Ni ya kibinafsi. Mara moja nikaamua kuikodisha. Kwa Sasa vyumba vyote vinne vimesheheni wageni na donge nipatalo kila siku tangu sherehe ianze Ni no kwelikweli. Kwa hakika nimepona kufuatia ujio Wa Hawa wageni wanaohudhuria tamasha ya mwaka huu ya utamaduni wa Lamu,” akasema Bw Ali Yusuf, mkazi wa mtaa Wa Langoni mjini Lamu.

Wachuuzi wa rejareja nao walikiri kuuza bidhaa nyingi kipindi chote cha Tamasha ya Utamaduni wa Lamu ikilinganishwa na nyakati za kawaida.

Samson Mwangi anayeuza vitu vya watoto kuchezea na mapambo anasema shehena za bidhaa alizouza siku mbili za tamasha ya utamaduni ni sawa na idadi ya bidhaa ambazo angeuza kwa kipindi cha karibu miezi miwili.

“Tamasha limenoga kibiashara si haba. Nimeuza na kuzoa faida kubwa na ninaendelea kuuza bado kwani tamasha bado linaendelea. Wateja Ni wengi kipindi hiki cha sherehe kinyume na siku za kawaida,” akasema Bw Mwangi.

Baadhi ya wenyeji,wageni na watalii waliohojiwa Jumamosi waliomba Tamasha ya Utamaduni wa Lamu iongezwe siku,wakidai siku tatu ni chache mno.

“Tamasha ya Utamaduni wa Lamu hutusaidia kuondoa msongo wa mawazo wa mwaka mzima. Isitoshe,kila sekta,iwe ni ya biashara ya uchukuzi, bidhaa madukani,rejareja,utalii,hoteli,gesti,uvuvi na nyingine nyingi, zote hunoga kipindi hiki cha tamasha ya utamaduni wa Lamu. Kwa nini sherehe kama hizi ziadhimishwe siku tatu pekee? Twaiomba serikali ya kaunti na wafadhili wazingatie kuongeza muda wa Maadhimisho ya tamasha hii kutoka siku tatu Hadi angalau siku 10,” akasema Bw Abdallah Shee, mkazi wa kisiwa cha Lamu.

Jumamosi waliohudhuria sherehe walipata fursa kujionea fainali za mbio za punda zilizoandaliwa alfajiri na mapema.

Pia walitumbuizwa kwa nyimbo za Taarab na ngoma za kitamaduni.

Alasiri kutakuwa na fainali za mbio za jahazi kwenye Bahari Hindi, uogeleaji, miongoni mwa michezo mingine kabla ya tamasha kusindikizwa na hafla ya kuwazawadi washindi eneo la Mkunguni kisiwani Lamu.

Kilele cha tamasha hizo ni Jumamosi usiku ambapo kutakuwa na tumbuizo kali kutoka kwa msanii wa Bongo Flava, Jay Melody atakayewabamba mashabiki wake, wageni na watalii mpaka chee eneo la Mkunguni.

  • Tags

You can share this post!

Kenya kuvaana na Ufaransa mashindano ya Rugby League jijini...

Beki Dorcas Shikobe roho juu Stars wakielekea Gaborone kwa...

T L