• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Kenya kuvaana na Ufaransa mashindano ya Rugby League jijini Nairobi

Kenya kuvaana na Ufaransa mashindano ya Rugby League jijini Nairobi

Na GEOFFREY ANENE

KENYA na Ufaransa zimetaja vikosi tayari kupepetana katika mashindano ya raga ya mataifa mawili ya Shirikisho la Kimataifa la Rugby League (IRL).

Mechi hizo zitasakatwa Desemba 2 na Desemba 5 ugani Jamhuri ASK jijini Nairobi.

Wafaransa wanaorodheshwa katika nafasi ya tisa kwenye viwango bora vya dunia vya IRL nao Wakenya wanapatikana nambari 31.

Wakenya wanatarajiwa kuwa na kibarua kigumu katika michuano hiyo wanayocheza baada ya kupepetwa na nambari 26 duniani Afrika Kusini 82-2 na 56-12 mjini Pretoria majuma mawili yaliyopita.

Ni mara ya kwanza kabisa Kenya inakutana na timu kutoka Bara Ulaya na pia inayoorodheshwa juu kabisa kama Ufaransa.

“Tunasubiri kwa hamu kubwa kusakata raga mbele ya mashabiki wetu na michuano miwili dhidi ya Ufaransa itakayopatia vijana wetu uzoefu zaidi,” amesema kocha wa Kenya, Edward Rombo.

“Bila shaka, mechi zaidi za kiwango hiki cha juu zitaimarisha ukuaji wa Rugby League nchini Kenya na kutuonyesha mahali tumefika katika ulingo wa mchezo huu duniani tunapotumai kuwania tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia siku moja,” aliongeza Rombo.

Timu ya Ufaransa imejaa wachezaji wanaocheza ligi ya malipo. Kocha Maxime Greseque amesema kuwa lengo lao nikupatia kila mchezaji fursa ya kucheza katika mechi zote mbili na wanasubiri kwa ari kusaidia katika ukuaji wa mchezo huu nchini Kenya.

Nahodha wa timu ya Kenya, Denish Ndinya, aliongeza, “Kuwa mwenyeji wa Ufaransa ni jukwaa jingine la kukuza Rugby League. Michuano hii itatusaidia kupima idadi ya wachezaji tuko nao na kuimarisha timu ya taifa na pengine kufungulia vijana milango ya kucheza raga ya malipo na pia kuvutia wadhamini zaidi kusaidia mchezo huu,” alisema.

Vikosi:

Kenya – Denish Ndinya (AP Warriors), James Odhiambo (AP Warriors), Malcom Busuru (AP Warriors), Sollo Mbugua (AP Warriors), Wycliffe Ratemo (AP Warriors), Joseph Biar (Ruffians), Victor Ndung’u (Ruffians), Anderson Oduor (Rhynos), Raymond Nyongesa (Rhynos), Saidi Abdalla (Rhynos), Michael Karani (Sharks), Edwin Watulo (Wolves), Evans Omondi (Wolves), Frank Awuor Otieno (Wolves), Joseph Otieno (Wolves), Kelly Omari (Wolves), Paul Seda (Winam), Ramadhan Masete (Winam)

Ufaransa – Baptiste Fabre, Mathias Leveille, Nittim Pedrero (Albi); Maxime Grosson, Baptiste Pourchi (Avignon); Felix Aubry, Clement Boyer, Clement Herrero, Nolan Lopez-Buttignol (Carcassonne); Bastien Scimone (Dragons); Quentin Crunel, Paolo Dallasta (Limoux); Allan Baby, Mathias Marty (Pia); Guillermo Aispuro-Bichet, Yacine Ben Abdeslem, Corentin Le Cam (St Esteve XIII Catalan); Hnaloan Hnangan, Mathieu Pons (St Gaudens); Wail Skoundri (Toulouse).

  • Tags

You can share this post!

Watu watano wapoteza maisha kwenye ajali mjini Molo

Wageni wataabika kupata vyumba vya kulala kipindi kizima...

T L