• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 5:50 AM
Wahubiri jijini Nairobi kuendelea kueneza Neno bila kutozwa ada

Wahubiri jijini Nairobi kuendelea kueneza Neno bila kutozwa ada

NA WINNIE ONYANDO

WAHUBIRI na wasanii wanaotumia bustani mbalimbali katika Kaunti ya Nairobi wamepata afueni baada ya serikali ya kaunti hiyo kuamua kutupilia mbali mpango wake wa awali wa kuwatoza ada za kila siku.

Sheria ya Fedha ya 2023, iliyotiwa saini na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja wiki jana inaonyesha kwamba watakaohubiri katika bustani za Jeevanjee, Uhuru Park, na maeneo mengine ya umma, hawatatozwa.

Kulingana na Sheria, wahubiri hao hawatatozwa tena malipo ya kila siku kwa shughuli zao.

Hapo awali, mswada wa fedha ulipendekeza wahubiri hao watozwe ada ya kila siku ya Sh500 kuhubiri katika bustani mbalimbali.

Mapato yaliyokusudiwa kutoka kwa ada hizi yalikuwa sehemu ya juhudi za serikali ya kaunti kukusanya Sh19.99 bilioni kutoka kwa rasilimali zake, kama ilivyoainishwa katika mpango wa Bajeti ya 2023/2024.

Wahubiri katika bustani za Uhuru Park na Central Park pia wangetakiwa kulipa Sh1,000 kila siku kabla ya kuruhusiwa kueneza ujumbe wao katika bustani hizo.

Kuhusiana na hilo, serikali ya kaunti pia imepunguza malipo ya kila siku kwa wasanii wanaonuia kurekodi video hadi Sh2,500 ikilinganishwa na Sh5,000 zilizopendekezwa hapo awali.

Ada ya kuandaa tamasha kwa siku katika viwanja vya Uhuru Park na Central Park imepunguzwa kutoka Sh50,000 za awali hadi Sh40,000.

Zaidi ya hayo, ada ya kuegesha magari imesalia kuwa Sh200.

Kadhalika, gharama ya vibanda na nyumba za biashara imepandishwa kwa asilimia 10.

Gavana Sakaja baada ya kutia saini mswada huo wa fedha kuwa sheria alisema kuwa sheria hiyo itaisaidia serikali yake kutekeleza baadhi ya ahadi alizotoa.

“Namashukuru sana Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Ken Ngondi na madiwani wote wa Nairobi kwa kupiga kura kuunga mswada huo wa fedha 2023,” alisema Gavana Sakaja.

  • Tags

You can share this post!

Kamati ya Seneti yajitetea ikisema haikudandia pesa za...

Kindiki atoa majina na picha za washukiwa wakuu wa...

T L