• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:47 PM
Kamati ya Seneti yajitetea ikisema haikudandia pesa za Pasta Ezekiel kuenda kujionea Kanisa la Mavueni

Kamati ya Seneti yajitetea ikisema haikudandia pesa za Pasta Ezekiel kuenda kujionea Kanisa la Mavueni

NA MARY WANGARI

MWENYEKITI wa Kamati Maalum ya Seneti inayochunguza mauaji katika msitu wa Shakahola, Danson Mungatana, amekanusha madai kuwa ziara ya maseneta katika Kaunti ya Kilifi ilifadhiliwa na Pasta Ezekiel Odero, anayehusishwa na mhubiri Paul Mackenzie.

Mnamo Jumatatu, wanachama 11 wa Kamati hiyo wakiongozwa na Seneta huyo wa Tana River, walizuru kanisa la Pasta Ezekiel la New Life Prayer Centre and Church lililopo eneo la Mavueni, Kaunti ya Kilifi, huku maswali yakizuka kuhusu ziara hiyo.

Akihutubia wanahabari Jumanne kwenye Majengo ya Bunge, seneta Mungatana alifafanua kuwa walizuru kanisa la Pasta Ezekiel kwa lengo la kubaini ukweli kuhusu masuala nyeti yaliyotajwa kwenye uchunguzi huo.

Haya yamejiri siku moja tu baada ya timu ya maseneta kukubali mwaliko wa Pasta Ezekiel katika kanisa lake ambapo aliahidi kugharimia matumizi ya maseneta wote ambao wangeshiriki ziara hiyo, alipofika kujibu maswali mbele ya Seneti.

“Nitalipa mje muone yale tunayofanya. Ninaomba kwa dhati kwamba Mwenyekiti wa Kamati atawashawishi wanachama waje,” alisema Pasta Ezekiel katika kikao hicho.

Maseneta waliokubali mwaliko wa Pasta Ezekiel ni pamoja na Eddy Oketch (Migori) Hillary Sigei (Bomet) Richard Onyonka (Kisii), David Wakoli (Bungoma) Abdul Haji (Garissa), William Cheptumo (Baringo) na maseneta maalum Tabitha Mutinda, Hamida Kibwana, Shakila Mohamed na Veronica Maina.

Kulingana na Bw Mungatana, ziara yao katika makao makuu ya Pasta Ezekiel iliwezesha kamati hiyo kubaini ukweli kuhusu maswala kadhaa yaliyowasilishwa ikiwemo kuwepo mochari na makaburi katika kanisa hilo.

“Mlikuwa hapa wakati Pasta Ezekiel Odero alitualika akisema njooni muone. Kulikuwa na madai sugu jinsi mlivyoona kwamba kuna makaburi… tulienda kujione… kuwa kuna mochari… tulienda kujionea. Ilidaiwa pia kuna uhusiano kati yake na Mackenzie hivyo wanahubiri kuhusu kujinyima chakula ili kumuona Yesu. Tulipozuru hapo tuliona mkahawa hivyo unapata taswira tofauti. Mahali palipodaiwa kuwa mochari tulikuta ni chumba cha jenereta ya kusambazia nishati. Makaburi yaliyodaiwa tulipata ni eneo la ujenzi,” alifafanua Bw Mungatana.

Kuhusu iwapo Bw Ezekiel yuko na hatia au la, seneta Mungatana alifafanua kuwa Kamati hiyo haina mamlaka ya kufanya uamuzi huo.

Alifafanua kuwa lengo kuu la Kamati hiyo lilikuwa kuchunguza madai kuhusu Pasta Mackenzie na wala si kuhusu Ezekiel.

Kando na kuzuru Kanisa la Pasta Ezekiel ambapo walipangiwa kushiriki kikao na viongozi wa kanisa hilo, seneta Mungatana alifichua kuwa Kamati hiyo ilipata fursa ya kukutana na Kamati ya Usalama katika eneo hilo.

“Baada ya mkutano wetu naye, tulitumia fursa hiyo kukutana na Kamati ya Usalama ya Kilifi lakini mkutano huo vilevile ulikuwa kupitia kamera. Hivyo tulipata fursa nyingine ya kujadili masuala kwa mtazamo tofauti na kuboresha ripoti yetu,” akamalizia.

  • Tags

You can share this post!

Juhudi kuhifadhi na kukuza vyakula vya kiasili 

Wahubiri jijini Nairobi kuendelea kueneza Neno bila kutozwa...

T L