• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 PM
Kindiki atoa majina na picha za washukiwa wakuu wa mashambulio ya kigaidi Lamu

Kindiki atoa majina na picha za washukiwa wakuu wa mashambulio ya kigaidi Lamu

NA CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Usalama wa Ndani Profesa Kithure Kindiki ametoa majina na picha za washukiwa 35 ambao ni wa kundi la Al-Shabaab linalowahangaisha sana wakazi wa Boni na Lamu kwa ujumla.

Kwenye taarifa aliyoitoa Jumanne, Oktoba 17, 2023, waziri Kindiki alisema kuwa washukiwa hao wanahusishwa na utekaji wa vilipuzi ardhini, mauaji ya raia na utekelezaji wa shambulio katika kambi ya kijeshi ya Amerika eneo la Manda mnamo 2020.

“Wizara ya Usalama wa Ndani itachapisha rasmi majina ya washukiwa hao ambao tunawachukuliwa kama wapangaji wakuu wa mashambulio hayo, na wanaohusika zaidi katika ufadhili na utekelezaji wa mashambulio hayo,” akasema Prof Kindiki.

Orodha ya watu hao inajumuisha watu ambao ni raia wa Kenya na wengine ambao ni wageni.

Wizara hiyo sasa imeanika wazi picha za washukiwa hao.

Watu hao ni Maalim Ayman, Ramadhan Kioko, Abdullahi Banati, Andreas Martin Muller, Abu Amar, Suleiman Maktum, Yusuf Anau (Raia wa Tanzania), Abdiweli Yassin Isse, Idris Dhul Kifir, Silla, Ibrahim Magag, HassaneTijana na Fahad ambaye ni raia wa Bangladesh.

Wengine ni; raia wa Tanzania Jamalo, Sheikh Nganglangalam, Janagale Huteiba (raia wa Ethiopia), Bashir Mursal Mohamud, Abu Khatal, Maalik Alim Jone kutoka Uingereza, Abu Said, Abu Anan, Mzee Mashella, Warsame Ali, Mohamed Mwanjama Salim na Abdikhadir.

“Tunatoa notisi kwa wahalifu hao kujisalimisha katika kituo cha polisi kilichoko karibu au katika kambi ya chifu. Ikiwa hawatajisalimisha, tutawatafuta na kuwatendea kile ambacho tunapaswa kuwatendea kwa mujibu wa sheria,” Prof Kindiki akaeleza.

Waziri alitoa wito kwa umma kutoa habari kuhusu waliko wahalifu hao akisema serikali itatoa zawadi ya kifedha kwa habari zitakazosaidia kukamatwa kwa washukiwa hao.

Washukiwa hao pia wamehusishwa na utegaji wa vilipuzi vya kujitengenezea kwenye barabara na kuchangia kuuawa kwa raia katika barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen, mauaji ya raia katika maeneo ya Lango la Simba, Witu na Mpeketoni, miongoni mwa maeneo mengine.

  • Tags

You can share this post!

Wahubiri jijini Nairobi kuendelea kueneza Neno bila kutozwa...

Linturi akemea Nacada akisema miraa, muguka si dawa za...

T L