• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 2:29 PM
Wakazi kuumia upya kaunti ikiongeza ada ya kuwakusanyia takataka

Wakazi kuumia upya kaunti ikiongeza ada ya kuwakusanyia takataka

WINNIE ATIENO NA FARHIYA HUSSEIN

WAKAZI wa Mombasa kwa sasa watalazimika kulipia Sh500 kila mwezi kutoka Sh200 walizokuwa wakilipa awali kwa ajili ya huduma ya kukusanya takataka.

Hii ni baada ya Kaunti ya Mombasa kukubali mabadiliko ya mswada wa kaunti wa kusimamia takataka 2023. Kukubaliwa kwa mabadiliko hayo sasa kutachangia mabadiliko kwa sheria ya Kaunti ya Mombasa ya kusimamia takataka 2021.

Gavana Abdulswamad Nassir tayari alikuwa ametia saini sheria hiyo ambayo itahitaji pia meli zinazotia nanga katika bandari ya Mombasa kutozwa Sh300 kwa kila tani 100. Kiwango cha chini kitakachotozwa meli ni Sh30,000.

Badiliko jingine muhimu ni ongezeko la tozo ya kukusanywa kwa takataka. Kwa sasa nyumba zitalazimika kuongezea Sh300 kwa fedha walizokuwa wakilipa awali ili takatata nyumbani mwao zichukuliwe na kutupwa.

Mwenyekiti wa kamati ya mazingira na kusimamia takataka, Juma Kambi, alilazimishwa kuizindua upya mswada huo, ambao ulikuwa umepingwa mara mbili na MCAs. Sera hiyo ilitupwa nje mara ya kwanza wabunge wakieleza sababu zao ikiwemo gharama ya juu ya maisha.

Vikao vya bunge vilibidi viahirishwe baada ya wabunge hao kutofautiana kuhusu tozo hiyo.

“Sheria hii inalenga kubadilisha sheria ya Kaunti ya Mombasa ya kusimamia takataka ya 2021 ili iongeze tozo ya kukusanya takataka kutoka kwa kila nyumba kwenye makazi,” ikasoma sehemu ya notisi iliyochapishwa katika gazeti rasmi la kiserikali.

Mwakilishi wadi wa wadi ya Shika Adabu alilitaka bunge hilo kuunga mkono uchapishaji wa mswada huo ili iwasilishwe kwa bunge.

Wiki iliyopita, baadhi ya MCAs walipigana masumbwi katika bunge hilo kuhusiana na mswada huo, wengine wakionya kuwa malipo hayo yangewatwika mzigo mzito wakazi wa Mombasa.

“Hii si haki. Hatuwezi endelea kuwaadhibu wakazi kupitia ushuru. Mswada huu utatuumiza sisi sasa na tutalipia ifikapo 2027 tutakapokuwa tukirudi kwa wakazi kuomba kura. Tuwe na ubinadamu,”akasema mbunge mmoja ambaye aliombwa asitajwe.

Licha ya hayo, wabunge waliosalia walishikilia msimamo kuwa, mswada huo uliokuwa umeandaliwa na serikali ulikuwa lazima upitishwe.

“Kama washikadau wa sekta hiyo, tumeachwa nje katika mchakato mzima wa kuandaa mswada huo. Maoni yetu hayakujumlishwa kabla ya kupitishwa. Mkazi wa Bangladeshhawezi kulazimishwa kulipa Sh 500 kama yule wa eneo la Nyali. Tunataka mswada huo uorodheshe nyumba kulingana na mapato yao,” akasema mwanaharakati wa mazingira Bw Alfred Sigo.

Alimtaka Bw Nassir kuwahusisha washikadau wote wa sekta ya usimamiajin wa takataka wakiwemo wanaokusanya takataka hizo ambao hutegemea kazi hiyo kujisakia tonge.

  • Tags

You can share this post!

Bingwa wa riadha za wakongwe Sikuku atangaza kuvizia rekodi...

Serikali yatangaza kusimamisha kazi maafisa wakuu sita wa...

T L