• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 5:50 AM
Wawili waponea kifo baada ya pikipiki kuingia kwenye shimo lililojaa matope

Wawili waponea kifo baada ya pikipiki kuingia kwenye shimo lililojaa matope

Na SAMMY KIMATU

WATU wawili waliponea kifo kwa tundu la sindano walipohusika kwenye ajali ya barabara katika mtaa mmoja wa mabanda katika Kaunti ya Nairobi, jana Jumapili.

Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Crescent lililoko kwenye mtaa wa mabanda wa Kayaba, kaunti ndogo ya Starehe.

Katika kisa hicho, mwendeshaji wa pikipiki ya bodaboda na mteja wake walitumbukia ndani ya shimo baada ya pikipiki kugonga Tuktuk iliyokuwa imesimama barabarani.

Mwenyekiti wa usalama mtaani humo, Bw Jacob Ibrahim, alisema ajali hiyo ilitokea baada ya dereva wa pikipiki ya bodaboda kugonga Tuktuk akijaribu kuipita.

“Pikipiki iligonga Tuktuk wakati mwendeshaji akijaribu kupitia upande wa kushoto. Kutokana na wembamba wa barabara, waliteleza kutoka barabarani na kutumbukia ndani ya shimo lililojaa matope,” Bw Jacob akasema.

Wakazi waliokuwa katika shughuli zao za kila siku walifika haraka penye tukio baada ya mwanamke kupiga kamsa.

Vijana waliokoa mwendeshaji bodaboda, mwanamke pamoja na sanduku lake lililokuwa na nguo baada ya kufunguka walipoanguka.

Akinamama waliokuwa wakipika chakula cha kuchuuza walimchukua mwanamke aliyejaa matope mwilini, wakamwombea bafu katika kilabu kimoja karibu na eneo la kisa ili aoge na kubadilisha nguo.

“Mwanamke alionekana kushtushwa na ajali. Tulimwosha kwani hakujielewa. Alipobadilisha nguo tulimpeleka kupatiwa huduma ya kwanza katika zahanati moja mtaani,” Mama aliyejitambulisha kwa jina moja Mama Wangari akasema.

Bw Jacob alieleza kwamba pikipiki ilikuwa ikimsafirisha mwanamke kutoka South B kuelekea mtaa wa mabanda wa Tetrapak.

Vile vile, eneo la ajali ni mahali mradi wa ujenzi wa barabara ya lami unaendelea huku barabara ya muda iliyopo ikiwa ni nyembamba.

“Barabara iliyopo kwa sasa ni ya kutumiwa na gari moja pekee. Ninawasihi wanaotumia barabara hii wawe waangalifu sana kwa sababu kando yake kuna mashimo ya kina kirefu na yamejaa matope,” Bw Jacob akashauri.

You can share this post!

OKA wakataa presha ya Uhuru

Jinsi ya kuandaa milkshake ya tende

T L